Wachungaji
watatu wamenusurika kipigo kutoka kwa wananchi, baada ya kushindwa
kumfufua marehemu katika Kijiji cha Sitalike Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya
Mpanda mkoani Katavi.
Wachungaji
hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa wanao uwezo wa kumfufua
marehemu mwanakijiji mwenzao aliyefariki dunia hivi karibuni na kuzikwa
kwenye makaburi ya Kijiji hicho.
Akisimulia
tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Angelo, alisema
kuwa tukio hilo lililovuta hisia za watu wengi lilitokea Mei 7, majira
ya saa 4 za asubuhi kijijini hapo.
Alisema
kuwa wachungaji hao ambao walikuwa watatu walifika kwenye ofisi ya
Kijiji na kujitambulisha kuwa wao ni wachungaji wanatoka katika Kijiji
cha Nsimbo na watakuwapo kijijini hapo wakiwa wameitwa na ndugu wa
marehemu, Raymond Mirambo aliyefariki dunia siku moja na kuzikwa
kijijini hapo.
Alisema
wachungaji hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa wanataka kufanya
maajabu ambayo ni ya kihistoria nchini ya kufanya maombi mfululizo na
kumfufua marehemu Raymond.
Mwenyekiti
huyo alisema kutokana na kujitambulisha kwa wachungaji hao kwenye ofisi
ya kijiji, uongozi wa kijiji uliwaruhusu wachungaji hao kufanya maombi
hayo ya kumfufua marehemu huyo.
Alisema
baada ya kuruhusiwa na uongozi wa kijiji walielekea nyumbani kwa
marehemu na kuwakuta ndugu wakiwa wanawasubiri kwa ajili ya maombi hayo
ya kumfufua ndugu yao.
Alisema
maombi hayo yaliendelea kwa muda wa siku saba usiku na mchana pasipo
kuwa na mafanikio yoyote, hali ambayo iliwafanya ndugu wa marehemu
washikwe na hasira.
“Wananchi,
ndugu na jamaa walikasirika kutokana na kuona kuwa wachungaji hao
wanawatapeli na kwa sababu waliwasababishia kuingia gharama kubwa ya
kulisha watu waliokuwa wakishiriki maombi hayo,” alisema.
Kwa
mujibu wa Angelo, baada ya kuona hafufuki, ndugu wakiongozwa na mama
mzazi wa marehemu waliamua kwenda kutoa taarifa ofisi ya kijiji, ili
kuepusha vurugu ambazo zilitaka kutokea.
Alisema
watu walioonekana kuwa na hasira kwa kutoona muujiza wa kumfufuka
marehemu walitaka kuwapiga wachungaji hao kwa kuwapotezea muda na
kuwatapeli.
Mwenyekiti
huyo alisema viongozi wa Kijiji baada ya kufika kwenye eneo hilo
walikuta ndugu wa marehemu wakiwa wanafoka kwa hasira huku wakiwa
wanawatuhumu wachungaji hao kuwa ni matapeli.
“Sisi
uongozi wa Kijiji tulikuta vurugu na wananchi walikuwa wanataka
kuwapiga wachungaji hao, tulichofanya kuepusha shari ni kuwaondoa
wachungaji hao eneo hilo na kwa kweli walitii agizo hilo na kuondoka
zao,” alisema Angelo.
Post A Comment: