Wednesday, 23 May 2018

Sugu alitetea Jeshi la Magereza Bungeni

Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi 'Sugu' amelitetea Jeshi la Magereza mbele ya  Bunge  kuwa jeshi hilo lina matatizo makubwa ya kiusafiri jambo ambalo linapelekea wafungwa kupelekwa Mahakamani kwa miguu kitendo ambacho kina hatarisha usalama wa mfungwa na askari kiujumla.

Kauli hiyo ya Sugu imetolewa jana  Mei 22, 2018 Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 34 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

"Pamoja na matatizo waliyokuwa nayo Jeshi la Polisi katika masuala ya vyombo vya usafiri lakini niwahakikishie Jeshi la Magereza lina hali mbaya sana, hawana magari sio tu magari mabovu hawana magari kabisa, kiasi kwamba wanafikia hatua ya kuwapeleka wafungwa ambao wanakesi Mahamani kwa miguu huku wakiwa wamewafunga pingu. Hii ni mbaya sana kwa usalama wa askari magereza pamoja na wale watuhumiwa ambao wamefungwa pingu", alisema Sugu.

Pamoja na hayo, Sugu aliendelea kwa kusema "mtu anatuhumiwa ujambazi halafu anapitishwa mtaani kwa miguu wananchi wanamuona, wanaweza wakamvamia na kumshambulia pamoja na kuhatarisha maisha ya mfungwa".

Kutokana na ushauri huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Mwigulu Nchemba akampongeza Mhe. Sugu kwa kusema "nimpongeze Mhe. Sugu kwa kuuliza swali kwa experience, na niseme kwamba yeye ni mshauri mzuri. Tutalizingatia hilo ili tuweke mgao kwenye upande wa Jeshi la Magereza ili kuepuka na tahadhari aliyosema".

No comments:

Post a comment