MKUU wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amemteua aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Uhalifu Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi, Maulid Makabila kuwa Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (D/DCI) Zanzibar, huku akifanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa.

Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi Mei 17, 2018 na Msemaji wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa imeeleza kuwa, katika mabadiliko hayo aliyekuwa DCI Zanzibar, Ramadhan Ng’anzi ameteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Charles  Mkumbo aliyehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi, Dar es Salaam.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali amehamishwa na kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba huku nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Thobias Sedoyeka aliyekuwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam.

Siku chache zilizopita Kamanda Nassir alizua gumzo mitaani na mitandaoni baada ya video yake kusambaa ikimuonyesha akiwapiga biti wanaume wanaojifanya kukohoa hasa wanapoona akina mama wenye makalio makubwa ‘wowowo’ wakipita mbele zao na kudai kufanya hivyo ni shambulio la aibu, huku akisema atakayefnya hivyo atakamatwa na kufikishwa mahakamani.

 “Kamanda wa  polisi mkoa wa Kusini Unguja, Makarani Khamisi amehamishiwa makao makuu ya upelelezi Zanzibar na nafasi yake kuchukuliwa na kamishna msaidizi wa polisi, Suleiman Hassan aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Kaskazini Unguja,” anasema Mwakalukwa katika taarifa hiyo.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Hasina Ramadhani Taufiq anakuwa Ofisa Mnadhimu Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi, Haji Abdallah Haji aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Mjini Magharibi.


Taarifa hiyo inaeleza mabadiliko hayo ni ya kawaida yenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: