Sunday, 27 May 2018

Polisi Dar Wakusanya Milioni 972 Za Makosa Barabarani Ndani ya Wiki Mbili

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekusanya Sh972.7 milioni za makosa ya usalama barabarani katika kipindi cha wiki mbili.

Katika operesheni hiyo ya ukamataji wa magari iliyofanyika kati ya Mei 11 hadi Mei 24, mwaka huu magari yaliyokamatwa ni 24,116, pikipiki 763 na daladala 10,301.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema, “Waendesha babodada waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia mishikaki (abiria zaidi ya mmoja) ni 59. Jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 30,850 na fedha zilizopatikana ni Sh972 milioni.

“Madereva na wamiliki wa magari wanatakiwa kulipa faini zao ndani ya siku saba ili kuepuka faini kuongezeka na kusababisha kukamatwa tena kwa kulimbikiza madeni,” alisema Mambosasa.

Katika hatua nyingine; Mambosasa alisema polisi wanamshikilia mhudumu wa Hoteli ya Sleep Inn kwa tuhuma za kukutwa na sare za polisi, silaha, cheo cha koplo, pingu na nguo inayofanana na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

“Tulipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu mmoja anatumia sare za polisi kuwakamata watu na kuwafunga pingu na kuwatishia bastola ili kufanikisha kupora mali maeneo mbalimbali ya Jiji. Baada ya kupata taarifa hizo tulianza ufuatiliaji na kuweka mtego. Mei 12 tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa,” alisema Mambosasa.

No comments:

Post a comment