Monday, 14 May 2018

Mkuu wa Wilaya ya Temeke aibiwa gari nyumbani kwake

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva, ameibiwa gari lake na watu wanaosadikiwa majambazi, nyumbani kwake Toangoma, jijini Dar es Salaam.

Lyaviva amesema ameshangazwa na wezi hao kupata ujasiri wa kwenda kuiba nyumbani kwake bila kujali nafasi yake ya uongozi ikiwamo ya   mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

”Yaani hata hawajaogopa kuja kuiba nyumbani kwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama na pia kulikuwa na walinzi wawili,’ alisema.

Akizungumzia tukio hilo, Lyaniva alisema wezi hao waliingia nyumbani kwake usiku wa kuamkia juzi kwa kukata uzio na walichukua gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 920 DMQ.

“Wakati wezi hao wanaingia sikuwapo, nilikuwa safari ya kikazi mkoani Dodoma lakini kulikuwa na watu nyumbani kwangu. Hata walinzi walikuwapo lakini wamesema hawajasikia,” alisema.

”Ninao walinzi wawili na wameniambia hawakusikia chochote lakini Kamanda (wa Polisi Mkoa wa Temeke) analifanyia kazi tukio hilo maana hata mimi sielewi vizuri. Ijumaa (juzi) nilipoingia nyumbani ndipo nikapatiwa hizo taarifa,” alisema.

No comments:

Post a comment