Kampuni ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.

Makubaliano hayo yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli Profesa Palamagamba Kabuni na  Mkurugenzi wa Tanzanite One Bw.Faisal Juma.

Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa  kamati ya majadiliano kwa upande wa Serikali, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzanite One imekubali kulipa fidia Serikali kutokana na mambo iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu ulioleta hasara kwa Serikali.

Amesema fidia hiyo inatakiwa kulipwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili kuanzia leo  na haitahusisha Kodi. Pia Kampuni hiyo Tanzanite One italazimika kulipa kodi kama kawaida inazodaiwa na Serikali na tozo nyingine zote zinazodaiwa na Serikali.

Pia  Serikali  imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa itafuata masharti yote ya sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni Watanzania tu ndio wanaoruhusiwa kuchimba madini ya Vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.

Aidha Prof. Kabudi amesema kuhusu wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzanite katika eneo la Mirerani  utaratibu mpya unawekwa lengo kubwa ikiwa ni kutekeleza sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo inalenga madini ya vito kuwa mikononi mwa Watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuunda kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za madini nchini ambapo wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia ikiwa ni mbali na malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo kodi.

Amesema Tanzanite One itahakikisha inafuata taratibu zote za Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kwa lengo la kuhakikisha rasilimali ya madini inawanufaisha Watanzania na kwamba uvunjifu wa sheria uliofanywa na kampuni hiyo hautajirudia tena.

“Sisi kama Tanzanite One tunaihakikishia Serikali kuwa uaminifu uliotuonyesha na sisi pia kama Kampuni tutahakikisha tunakuwa waaminifu na kuwa zao hili linanufaisha taifa kutokana na imani aliyotuonyesha Mhe. Rais kama wananchi wake kutupa nafasi na fursa ya kusikilizwa ili kurekebisha makosa tuliyoyatenda” amesema   Faisal.

Faisal amesema Tanzanite One itahakikisha haitafanya makosa iliyofanya mara ya kwanza na hivyo kuwa mfano wa kampuni nyingine za madini kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam
16 Mei, 2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: