Sunday, 20 May 2018

Jeshi la Polisi: Chanzo hatuwezi kujua ni lazima uchunguzi wa kitaalamu ufanyike


Kamanda wa Polisi mkoa wa Ilala, Salum Amdani  amesema kwamba Jeshi la Polisi linasubiri taarifa ya daktari kufahamu chanzo cha  kifo cha mwanafunzi Edward Kahitwa wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kilichotokea jana.

Kamanda Amdani amesema hayo leo Mei 20, 2018 katika mahojiano maalumu na EATV na kusema kuwa daktari ndiye atafanya uchunguzi wa mwili wa marehemu na kuongeza kuwa itachukua muda kufahamu chanzo cha kifo.

“Chanzo hatuwezi kujua kwasababu ni lazima uchunguzi wa kitaalamu ufanyike sisi tunachoweza kusema kwamba ni kweli mwili wa marehemu ulikutwa chumbani baada ya sisi kupokea taarifa tulikwenda pale tukauchukua kwa taarifa nyinginne za kiuchunguzi”

Kamanda huyo wa Ilala amesema serikali itakuja kutoa taarifa kamili ya chanzo cha kifo hicho baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitabibu na kuongeza kuwa kwasasa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Marehemu Edward Kahitwa alikuwa ni mwanafunzi wa  mwaka wa tatu katika katika shahada ya Famasia Chuo Kikuu cha Afya na sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS), mwili wake ulikutwa chumbani katika hosteli za Chuo hicho hapo jana mchana Mei 19, 2018.

No comments:

Post a comment