Jeshi la Polisi nchini limewaaga makamishna wa Polisi wawili ambao wamefikia umri wa kustaafu  kwa mujibu wa sheria.

Makamishna hao ni aliyekuwa Kamishna wa Polisi wa Fedha na Lojistiki, Clodwin Mtweve  ambaye baadaye aliteuliwa  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Katibu  Tawala wa Mkoa wa Mwanza nafasi ambayo ameitumikia hadi kustaafu kwake.

Mwingine ni aliyekuwa Kamishna wa  Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi wa Makosa ya Jinai, Alice Mapunda ambaye ndiye polisi wa kike wa kwanza kupandishwa cheo hadi kufikia cheo cha Kamishna kwa Jeshi la Polisi tangu uhuru.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Simon Sirro amesema kuwa  katika utumishi wao ndani na nje ya Jeshi la Polisi Makamishna hao walishika nyadhifa mbalimbali ikiwemo kushiriki kikamilifu katika operesheni mbalimbali za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa na kuliletea sifa Jeshi la Polisi Tanzania ndani na nje ya nchi.

Kutokana na mchango wao kwa taifa, makamishna hao wametakiwa kuendelea kuwa msaada kwa Jeshi la Polisi wakati wowote watakapohitajika kwa kutoa ushirikiano na ushauri wa kitaalam utakaosaidia kupunguza uhalifu hapa nchini.

Hafla ya kuwaaga makamishna hao imefanyika jana katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) kilichopo Kurasini kuanzia saa moja na nusu na palipambwa na gwaride na mayonesho mbalimbali ya kazi za Polisi.
Wastaafu hao Clodwin Mtweve na Alice Mapunda.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: