Sunday, 27 May 2018

Bodi za maji kufanyiwa ukaguzi maalum KilimanjaroNAIBU   Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji,  Emmanuel Kalobelo ametaka serikali kufanya ukaguzi maalumu wa mahesabu ya bodi za maji za wilaya ya Hai na Siha mkoani Kilimanjaro.

Kalobelo aliyasema hayo juzi, baada ya kutembelea miradi inayotekelezwa na bodi hizo na kisha kufanya mazungumzo na wadau wanaotoa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa wilaya hizo.

“Sera ya maji inasema bodi za maji zitasaidiana na serikali kuboresha miundombinu pamoja na kuhakikisha kuwa zinakaguliwa hesabu zake  na wakaguzi wa  serikali ili kujua uendeshaji wake, kwa maana hiyo mnapaswa kukaguliwa,”alisema

Bodi za maji zilizopo katika Wilaya za Hai na Siha ni Losaa, Kia, Uroki, Bomang’ombe,  Lyamungo, Umbwe Magadini, Makiwaru na Lawate, Fuka.

Dira ya taifa ya upatikanaji wa maji vjijini hadi kufikia mwaka 2025 ni kuhakikisha kiwango cha upatikanaji wa maji unafikia asilimia 90 na asilimia 100 katika maeneo ya mijini.

Katika maelekezo yake, alizitaka bodi hizo kufuata sheria zilizopo ikiwa ni pamoja na miongozo iliyowekwa na serikali ili kufanikisha kazi wanayoifanya ya kufikisha huduma hiyo kwenye jamii.

Pamoja na mambo mengine, ameziagiza bodi hizo kuhakikisha kuwa gharama za kuvuta maji nyumbani zinakuwa nafuu ili kila mwananchi aweze kumudu na kufikia malengo ya taifa la upatikanaji wa maji kwa vijijini.

Awali akitoa taarifa kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya maji, Mkurugenzi  mtendaji wa halmashauri ya wilaya Siha, Verial Juwal alisema wilaya hiyo ina bodi tatu zinazohudumia wakazi  zaidi  120,000 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 iliyofanyika katika kata 17  ambazo wananchi wanapata maji kwa  asilimia 84.

Hata hivyo,  mwenyekiti wa bodi ya maji ya Lyamungo na Umbwe,  Michael Mmasy alimhakikishia,  Naibu Katibu mkuu huyo kwamba wao kama wadau wa huduma hiyo, wataendelea kushirikiana na serikali kutoa huduma na wananchi wote kufikiwa na mtandao wa maji.

No comments:

Post a Comment