Monday, 14 May 2018

Anusurika kifo baada ya kujifungia kwenye kontena bandarini

Mkazi wa Miembeni mjini Unguja, Hassan Juma amenusurika kifo baada ya kutolewa ndani ya kontena alikojifungia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassri Ali alithibitisha tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo.

Msimamizi wa makontena katika Bandari ya Malindi, Ibrahim Abdallah jana alisema chanzo cha Hassan anayekadiriwa kuwa na miaka 30 kuingia kwenye kontena na kujifungia hakijajulikana.

Abdallah alisema wakiwa katika kazi zao za kila siku eneo hilo juzi saa moja asubuhi walisikia sauti ikitoka ndani ya kontena lililopo juu ya jingine na kuzua taharuki miongoni mwao ikidaiwa ‘nakufaa’.

Alisema mtu huyo aliashiria kuomba msaada na walimuuliza yeye ni nani na alijitaja jina.

“Baada ya kutaja jina tulifungua kontena hilo ambalo alikuwa amelifunga na kumtoa akiwa na hali mbaya kiafya, tulimpeleka Hospitali ya Mnazi Mmoja na kupatiwa huduma ya kwanza,” alisema.

Naye msemaji wa hospitali hiyo, Hassan Makame alisema katika hatua za awali wamempatia huduma ya kwanza ili kuhakikisha hali yake inarejea kawaida. Alisema hajafanyiwa vipimo kutokana na hali yake kuonekana kudhoofu.

“Tumemtia dripu ili apate nguvu ili kuendelea na huduma nyingine za vipimo,” alisema Makame.

Kuli katika bandari hiyo, Mohamed Khamis Makame alisema ni mara ya kwanza kutokea tukio la aina hiyo eneo hilo, hivyo wanapaswa kuimarisha ulinzi.

No comments:

Post a comment