Wednesday, 4 April 2018

RIPOTI INATISHA: WANAUME KUUA WAKE, WAPENZI WAO!


Leyla na mumewe.
Tukio la mauaji ya mke, Leyla Mtumwa almaarufu Ndaya (36) (pichani), linalodaiwa kufanywa na mumewe, Kema Salum Kasam­bula ‘Belly’ (38), wote raia wa Tanzania huko jijini London nchini Uingereza mwishoni mwa wiki iliyopita, limeibua matukio mengine ya sampuli hiyo nchini, ripoti ya Uwazi inatisha.

Leyla, mwenyeji wa Arusha ambaye ni mtoto wa mama maarufu jijini humo aitwaye Hidaya aliyeimbwa na mwa­namuziki wa Kongo, Pepe Kalle miaka ya 90, alidaiwa kuuawa kwa kuchomwa visu na mumewe huyo ambapo zoezi la michango lilikuwa likiendelea ili mwili wake ulete nchini kwa mazishi.

Mwanamke waliyeuawa na mumewe mwaka 2010 na kufichwa kwenye mti wa Mbuyu, Singinda.

Leyla alikutwa na umauti mara baada ya kurejea ny­umbani alfajiri akitokea disko ambapo aliingia kwenye ugomvi mkubwa na mume wake iki­aminika kuwa, mwanaume huyo hakupendezwa na kitendo cha mkewe kurudi nyumbani alfajiri akitokea kujirusha huku akiwa amelewa.

Mara baada ya kujiri kwa tukio hilo na mengine mengi ambayo Magazeti Pendwa ya Global Publishers yamekuwa yakiya­ripoti, Uwazi liliingia mzigoni kutafuta ni nini chanzo hasa cha mauaji mengi ya aina hiyo na kuibuka na sababu saba;

…Aliyemuua mama mkwe wake na kumjeruhi mkewe kisha naye kujiua kwa kujifungia ndani ya nyumba na kuiteketeza kwa moto, Ngara.

MOJA: USALITI
Katika mahojiano na Mtaalam wa Saikolojia ambaye ni Mha­dhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Chris Mauki alisema kuwa, tafiti zote zilizofanywa na wao kama wanasaikolojia zilionesha kuwa suala la usaliti ndiyo chanzo kikuu cha mauaji hayo.

“Suala la usaliti limekuwa sugu, lakini na lenyewe linach­angiwa na mambo mengi, nayo ni mada ya kujitegemea kama vile wanandoa kushindwa ku­timiza wajibu wao wa kindoa.

“Utafiti pia unaonesha kwamba, ni wanaume wach­ache mno au wenye uwezo wa kusamehe na kusahau mara baada ya kuwafumania wake zao. Kinyume na wanawake ambao huweza kumfumania mume na akaombwa msa­maha yakaisha. Ile hasira ya mume kumfumania mkewe na kushindwa kujizuia ndipo hujikuta akitekeleza mauaji,” alisema Dk Mauki na kuongeza:
“Kama wanandoa hawa­takuwa makini na suala la kusa­litiana na kuliacha kabisa, basi tutegemee majanga zaidi.”
Mhusika wa tukio hilo la mauaji Ngara.

MBILI: MALEZI YA WAZAZI
Kwa mujibu wa Dk Mauki, wanandoa wapo hatarini zaidi kuuana kutokana na manung’uniko, hasira, kutovumiliana, kufoka, kutukanana, kutoaminiana, kuwaziana mabaya badala ya mazuri, kujikweza kwa majivuno yasiyo na maana kutokana na malezi ambayo wahusika waliyapata kutoka kwa wazazi wao.
“Mathalan mke au mume wakati anakua alimshuhudia baba akimpiga na kumdhalili­sha mama hivyo suala hilo likajengeka kwenye akili zao na kuamini kuwa ndiyo tabia. Tabia mbaya hutokana na malezi hivyo wazazi hawana namna ya kukwepa lawama hizi,” alisema.
TATU: KUNYIMANA UNY­UMBA
Pia Dk Mauki alibainisha kwamba, tafiti zinaonesha kwamba kumekuwa na malalamiko ya wanaume kunyimwa unyumba bila sababu za msingi hivyo kuwa na dhamira kwamba huenda wanasalitiwa.
“Halisemwi waziwazi kwa sababu ni jambo la aibu kama vile mume kupigwa na mke, lakini hiyo ndiyo hali halisi. Ili kuondokana na hili ni vyema wanandoa mkaku­baliana ratiba za kupeana unyumba kwa kusikilizana. Kama mmoja ana tatizo, basi mwenzake amsikilize na kukubaliana, la sivyo mauaji haya yataendelea kushamiri,” alisema mtaalam huyo am­baye pia ni mhamasishaji wa jinsi ya kufikia mafanikio.


NNE: SIMU
“Hatukatai kwamba ni lazima tuenende na muda, lakini kama ukisikiliza migogoro au visa vingi vya wanandoa kuuana, basi utasikia alipiga au kupigiwa simu na mtu na kuongea naye kisirisiri wakati mwenzake akimfuatilia.
“Au utasikia alikuwa akichati muda mrefu na ana­poulizwa huweka visingizio ambavyo hukasirisha na ku­sababisha ugomvi,” alisema na kuongeza:

TANO: MASLAHI
“Jambo lingine ambalo lime­kuwa likileta shida ni kwamba wanandoa wengi huingia kwenye ndoa kimaslahi.
“Utakuta mwanamke anapanga kabisa na kutumia nguvu nyingi ili aolewe na mwanaume mwenye uwezo akiamini kuwa mali alizonazo mwanaume huyo naye atazi­faidi. Sasa anapoingia ndani na kuonesha uchu huo, hapo ndipo hitilafu hutokea na ku­jikuta mmoja akipanga mbinu ya kumuondoa mwenzake kwenye himaya yake.”

SITA: KUKOSEKANA UPENDO WA DHATI
“Lakini yote kwa yote, tunapozungumzia taasisi ya ndoa kuna changamoto nyingi kama nilivyosema na mhimili mkubwa ni up­endo wa dhati. Hicho ndicho kimekosekana kwa baadhi ya wanandoa.
“Palipo na upendo tuta­vumiliana, tutasameheana, tutabebeana mizigo na tutahurumiana. Cha msingi ni wanandoa kutumia mbinu zozote zile kuhakikisha upendo haukauki ndani ya ndoa.”


SABA: KUKOSEKANA WA HOFU YA MUNGU
Mbali na Dk Mauki, Uwazi lilizungumza na viongozi wa dini ambao ambao wote walisema kuwa chanzo kikuu cha kuongezeka kwa matukio hayo ni ukosefu wa hofu ya Mungu.
“Ndoa ni jambo la kimungu, anapokosekana Mungu miongoni mwa wanandoa, mambo hayo hayana budi kutamalaki kwa sababu ni rahisi mno shetani kuwata­wala. Ni vyema wanandoa wakaweka utaratibu wa kuzi­huisha ndoa zao kwa maombi na wakati mwingine kufunga na kuomba ili kuimarika na kumdhoofisha shetani,” al­isema Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la The World of Rec­onciliation Ministries (WRM) la Ukonga Ukonga jijini Dar, Nabii Nicolaus Suguye.

 “Ni kweli hali inatisha…wanan­doa wengi wanasahau kwamba walikula kiapo kuwa watakuwa mwili mmoja kwa sababu wam­emuweka kando Mungu wao, tumrudieni Mungu maana sisi ni wake ili atuondolee dhambi hii. Usiue ni agizo la Mungu mwenyewe na ni dhambi,” alisema Nabii James Nyakia wa Kanisa la Jerusalem lilipo Kinyantira jijini Dar.
Akizungumzia hali hiyo, Mku­rugenzi wa Chama Cha Wajane Tanzania (Tawia), Rose Sarwat alisema kuwa, mauaji miongoni mwa wanandoa yanayoelezwa kusababishwa na wivu wa ki­mapenzi ni matokeo ya baadhi ya watu kuingia katika ndoa kwa ku­vutwa na maslahi binafsi badala ya upendo.
“Wengi wanaingia kwenye ndoa wakisukumwa na maslahi binafsi na kwamba kuna kitu anakwenda kukipata hivyo mambo yakiwa tofauti anaamua kufanya lolote kwa sababu anakosa kufikia matarajio,” alisema Rose.
MBALI NA LEYLA
Mbali na Leyla, Uwazi lina ripoti ya kutisha juu ya mauaji ya aina hiyo likiwemo tukio la mume ali­yefahamika kwa jina la Maximil­ian aliyempiga risasi na kumuua mkewe kisha naye kujiua kwa risasi lililojiri Mei, mwaka jana jijini Mwanza.
Hivi karibuni, mwanaume mwingine aliyejulikana kwa jina la Diblo alidaiwa kumuua mkewe Herieth akiwa ukweni maeneo ya Koroni, Vingunguti jijini Dar.
Pia mwishoni mwa mwaka jana, mume aliyetambulika kwa jina la Matau Ngosha alidaiwa kumuua mkewe, Upendo Jonath­an huko Nyakasanga, Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar.
Katika tukio lingine, miezi kad­haa iliyopita, mume aliyetambuli­wa kwa jina la Fidelis Buberwa, mkazi wa Tabata jijini, Dar alid­aiwa kumshushia kipigo mkewe, Beatrice Kiriho na kumsababishia kifo kwa kosa la kuchelewa kure­jea nyumbani kutoka harusini.
Mapema mwaka huu, ali­yekuwa Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Ami Lukule alid­aiwa kumuua kwa kutumia jembe mkewe, Pendo Likule, kichanga chake, Joshua Ami na shemejiye wa kike, Magreth Samwel.
Tukio lingine la hivi karibuni, Polisi mkoani Katavi walimtia mbaroni mwanaume mmoja wa Kijiji cha Songambele Kata ya Sibwesa Tarafa ya Karema, Tan­ganyika kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa sababu ya wivu wa kimapenzi kisha kumzika huku mtoto wake mwenye umri wa miaka tisa akishuhudia tukio.
KUTOKA KWA MHARIRI WA UWAZI
Matukio haya ya kuuana mbali tu na kumkasirisha Mungu, yanatengeneza hofu miongoni mwa wanandoa hivyo ni vyema kila mmoja akajitahidi kuzizuia hasira zake pale anapokuwa ameudhiwa na mwenza wake na kuomba msamaha, kujishusha ni kati ya mambo yanaweza kuleta amani kwenye ndoa inapotokea mmekoseana.
Stori: WAANDISHI WETU,DAR

No comments:

Post a comment