Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa wito kwa serikali kufanya mazungumzo ya kitaifa kwa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii kujadili mustakabali wa amani na maridhiano ya kitaifa kabla hayajatokea makubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana  Alhamisi Aprili 5, Kaimu Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deodatus Balile alisema makundi hayo ni pamoja na wanahabari, viongozi wastaafu, wakuu wa vyama vya siasa na asasi za kiraia.

Ametaja makundi mengine ni vyama vya kitaaluma na vya makundi ya rika na makundi mengine muhimu kukutanishwa pamoja kama Rais John Magufuli alivyokutana na wafanyabiashara hivi karibuni.

“Hali ya nchi kwa sasa imekuwa na sintofahamu na malalamiko kutoka katika makundi mbalimbali jambo ambalo halitaleta afya kwa taifa, mambo mengi yamekuwa yakilalamikiwa ikiwa ni pamoja na kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni hasa kupitia vyombo vya habari kuzorota kwa demokrasia, ukuaji wa uchumi usioakisi hali halisi ya maisha ya watu.

“Tumeamua kutoa tamko hili leo, baada ya kukutana kwa wahariri jana kujadili mustakabali wa nchi na mambo yanayoendelea kwa sasa.

“Kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni imekuwa kikwazo kikubwa cha utendaji na ufanisi katika vyombo vya habari na kutokuwa huru kwa kutoa taarifa mbalimbali kama mwanzo na hofu huku ikiwafanya wananchi kusita kuzungumza,” alisema Balile.

Alisema mazingira ya kazi kwa wanahabari yamekuwa magumu kutokana na baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola kuwabughudhi na kufanya uovu wa wazi dhidi yao wanapokuwa kazini.

“Matukio mbalimbali ya Polisi kuwanyanyasa waandishi Wa habari yakiwamo ya wanahabari kunyang’anywa simu zao mfano yaliyotokea Dodoma kwa mwandishi kuporwa simu, kupotea kwa Azory Gwanda wa Mwananchi na kwingineko,” alisema Balile.

Amesema hali hiyo inawafanya waandishi na wananchi kuwa na hofu hasa kwa wale wa habari za uchunguzi.

“Vyombo vya habari vimekuwa vikifanya kazi katika mazingira magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na kuhojiwa na mamlaka kama vile Idara ya Habari (Maelezo) na Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Aidha, vituo vitano vya televisheni kutozwa faini ama kufungiwa vituo vitano vya televisheni kutozwa faini na TCRA  na kufungiwa kwa magazeti, baadhi ya adhabu zimekuwa zikitolewa kinyume na sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016,” alisema Balile.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: