Serikali imesemachanjo ya saratani ya shingo ya uzazi haizuii magonjwa ya kuambukiza yanayotokana na ngono zembe kama vile Ukimwi, kaswende na kisonono.

Kauli hiyo imetolewa jana bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Faharia Khamis Shomari.

Mbunge huyo alitaka kujua iwapo chanjo hiyo ya saratani inazuia magonjwa yatokanayo na ngono zembe kwa sababu vijana wanaanza kujihusisha na vitendo katika umri mdogo.

Akijibu swali hilo Dk. Ndungulile amesema serikali imezindua chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi  kwa kuanza na na mabinti wenye umri wa miaka 14.

“Baada ya hapo watafuata wa miaka tisa hadi 13. Aidha tafiti zimeonesha kuwa vijana wadogo wanajihusisha na ngono zembe hivyo niwaonye mabinti kuwa chanjo ya saratani ya shingo ya uzazi  haitawakinga dhidi ya magonjwa mengine ya kuambukiza kama ukimwi,  kaswende na kisonono,” alisema.

Aidha, ametoa rai kwa wabunge na wananchi wote kuwa chanjo hiyo ni salama na lengo la serikali ni kuhakikisha Taifa linaondokana  na tatizo la saratani ya shingo ya kizazi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: