Friday, 16 March 2018

Watanzania wadakwa na dawa za kulevya Kenya


Dar es Salaam. Watanzania watatu wamekamatwa Kenya wakidaiwa kukutwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya Sh1.9 bilioni.

Watuhumiwa hao ambao majina yao hayakutajwa walinaswa wakiwa katika hoteli moja mjini Mombasa huku dawa hizo zikiwa zimefichwa katika nguo zilizowekwa kwenye mabegi.

Kwa mujibu wa gazeti dada la Mwananchi, Daily Nation la Kenya, polisi walikuwa wakijiandaa kuwafikisha mahakamani. Waliingia nchini humo kwa usafiri wa basi wakitumia mpaka wa Lunga Lunga.

Dawa hizo zinadaiwa kuwa na uzito wa kilogramu 30.

Katika miaka ya hivi karibuni Kenya imekuwa ikichukua mkondo wa mataifa mengine duniani kukabiliana na mitandao inayosafirisha dawa za kulevya.

Mapema mwaka uliopita vyombo vya usalama vya Taifa hilo viliwakamata washukiwa 13 wa ulanguzi wa dawa za kulevya mjini Mombasa.

No comments:

Post a comment