Wednesday, 21 February 2018

Mkulima anaswa akiuza Bangi


Polisi walivyomnasa mkulima akiuza bangi
Polisi mkoani Manyara inamshikilia mkulima na mkazi wa Galapo, Emmy Nombo (62), kwa madai ya kujihusisha na biashara ya bangi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa, Augustino Senga, alisema tukio hilo lilitokea Alhamisi, majira ya 7:45 mchana katika Kijiji cha Mwada, wilayani Babati.

Alikamatwa akiwa na misoko 858 ya bangi sawa na kilo mbili na nusu.

“Askari wetu wakiwa doria walimtilia shaka mama huyo, askari wa kike wakamkagua na kumkuta ana bangi ambayo alikuwa ameifungia kwenye maungo yake,” alisema.

Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akisafiri kutoka Arusha kwenda Babati akiwa kwenye gari aina ya Toyota Noah.

“Ukimwaangalia huwezi kuamini kuwa anafanya biashara hii, hata hivyo, sisi hatuangalii umri, unadhifu wa mtu, cheo cha mtu, rangi, dini wala kabila kwa kuwa uhalifu hauangalii vitu hivyo,” alisema.

Alisema mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa ili kupata taarifa zaidi  zitakazosaidia polisi katika uchunguzi wake ikiwa ni pamoja na kuwabaini watu anaoshirikiana nao.

Kamanda Senga, alisema askari wake wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanapambana na wahalifu ambao watataka kuutumia mkoa huo kuwa ni  kichochoro cha kufanyia uhalifu au kupitisha bidhaa haramu

No comments:

Post a Comment