********************

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa siku tatu kwa dereva wa Roli aliye mwaga Kemikali aina ya Sulphur katika eneo la Msimba Tarafa ya Mikumi Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, kujisalimisha mara moja katika ofisi za NEMC zilipo Morogoro mjini kwani Kemikali hizo zimeanza kuleta madhara kwa wananchi waliokaribu na eneo hilo.

Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bwa. Jamali Baruti ametoa siku hizo baada ya kufika na kujionea namna wananchi wa eneo hilo walivyoathiriwa na kadhia hiyo.

NEMC imefikia hatua hiyo baada ya kupata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo, huku wananchi wakianza kupata madhara ikiwemo kuumwa macho, vichwa pamoja na kuwashwa kwa ngozi.

Bwa. Baruti amesema NEMC imesikitishwa na kitendo cha dereva wa roli hilo aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea nchi ya jirani ya Kongo kumwaga kemikali na kutokomea kusikojulikana huku ikiwa bado haijafahamika chanzo cha kuwepo kwa Sulphur hiyo kama ni ajali ama laa.

Katika hatua nyingine NEMC itamfuatilia na kumchukulia hatua dereva kwa kutokufuata Sheria ya Mazingira, kwani kitendo alichokifanya ni uharibifu wa mazingira huku wahanga wakubwa wakiwa ni wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo kwani Kemikali hiyo ina madhara makubwa kwa binadamu na mazingira kwa ujumla.

Sambamba na hayo NEMC inatoa rai kwa madereva wanaoendesha magari ya mizigo hususani wanaobeba Kemikali kufuata kanuni na miongozo ya ufungaji wa mizigo pamoja na kutumia vifungashio vinavyokidhi vigezo.

Kwa upande wao wananchi ambao ni mashuhuda wa tukio wamesema roli hilo lilidondosha Kemikali hizo usiku wa Januari mosi 2022 na kusababisha madhara kwa wananchi ikiwemo kuumwa na kichwa, macho na kifua hali ambayo imeleta sintofahamu kwa wakazi hao kwa kuhofia afya zao na kutokujua nini cha kufanya. Aidha walisema ukosefu wa elimu ndio chanzo cha kuathiriwa na Kemikali hizo huku wakiiomba Serikali kuwasaidia kupata matibabu ya haraka kunusuru afya zao.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: