Moja ya kivuko kilichowekwa pembezoni mwa barabara kuelekea katika makazi ya mtu kwenye eneo hilo.

Na Amiri Kilagalila, Njombe

BAADHI ya wananchi wa mtaa wa Ramadhani wanao ishi pembezoni mwa barabara kuu ya Njombe –Moronga inayojengwa kuelekea wilayani Makete,wamewalalamikia vibarua wanaokamilisha ujenzi kwenye barabara hiyo kwa kuwatoza shilingi elfu 10 hadi elfu 30 ili kuwekewa vivuko vya kuingia kwenye nyumba zao.

Malalamiko hayo yametolewa na wananchi wa mtaa wa Ramadhani Atu Masawe na Alfonce Sanga ambao wamesema kutokana na uhitaji wa vivuko vya kwenye barabara inayotengenezwa ya Njombe-Moronga wawekeji vivuko hivyo wanawataka wenye uhitaji kutoa kiasi hicho cha fedha ili wawekewe Vivuko.

“Wanasema hatupo kwenye orodha ya kuwekewa vivuko kwa hiyo kama tunataka tupate Vivuko tujiongeze na sisi kwa kuwa tuna shida wanasema tutoe elfu ishirini au therathini”alisema Atu Masawe

Alfonce Sanga alisema “Hawa vibarua wanatuchuja hela kuna wengine wamechukua elfu ishirini na wengine wanasema lete chochote,unawapelekea ndizi wanasema bado lete na hela kwa ajili ya vivuko cha ajabu tunakuta tunatozwa na hela na kama huna hela wanatoa wanaweka kwa mwingine”

Diwani wa kata ya Ramadhani bwana Nickson Nganyange amekili kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wananchi na kutaka wasitoe pesa yoyote kwani vivuko hivyo serikali ndiyo imegharamia.

“Vivuko hivi naamini vitaendelea kuwekwa na maeneo mengine yeyote,ninaomba wananchi wasitoe hata shilingi moja kwa ajili ya kuwekewa vivuko kwa kuwa vipo kwenye mkataba waliosaini na serikali kwa ajili ya kujenga hii barabara”alisema Nganyange

Mhandis Mshauri wa mradi wa barabara ya Njombe-Moronga Michael Funga amesema malalamiko hayo ya wananchi bado hayajamfikia ofisini kwake na kukemea tabia hiyo ambapo ameta wananchi kutoa taarifa ofisini kwake ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.

“Vivuko tunavyowawekea watu havitozwi hela,mtu yeyote atakayetozwa hela tungependa hayo malalamiko yaje kwetu na sisi tutapambana nao,huu mradi umefadhiliwa na serikali”alisema bwana Funga.

Barabara hii ya Njombe Moronga yenye urefu wa kilomita 53.9 inatekelezwa na Kampuni ya Crown Tech Consultant.
Share To:

Post A Comment: