Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akiziungumza wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira katika mgodi wa kati wa dhahabu wa Taichangxin uliopo katika Wilaya na Mkoa wa Geita

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira katika mgodi wa kati wa dhahabu wa Taichangxin uliopo katika Wilaya na Mkoa wa Geita Desemba 3, 2021. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Sinyamule.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akiangalia maji yanayotiririka wakati wa shughuli za uchenjuaji wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira katika mgodi wa kati wa dhahabu wa Taichangxin uliopo katika Wilaya na Mkoa wa Geita Desemba 3, 2021.

Bwawa la topesumu ambalo limejengwa na kuanza kutumika kabla ya kukaguliwa na kupewa cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

……………………………………………………….

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo ameelekeza wamiliki wa migodi midogo na ya kati inayotumia Zebaki na Cyanide katika uchenjuaji waache kutiririsha ovyo maji yenye sumu na badala yake wafuate taratibu za kimazingira ili kulinda maisha ya wananchi.

Jafo ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara katika mgodi wa kati wa Taichangxin uliopo katika Wilaya na Mkoa wa Geita ambapo ametoa siku 90 kwa uongozi wa mgodi huo kuzifanyia kazi changamoto za kimazingira zilizobainika.

Alisema kuwa hajaridhishwa na namna mgodi huo unaendeshwa kwa kushindwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa mazingira ikiwemo kujenga na kutumia shimo la takasumu bila kupata cheti cha tathmini ya athari kwa mazingira na kuacha maji yenye sumu kutiririka ovyo.

Waziri Jafo ameelekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa kuchukua hatua stahiki kwa uongozi wa mgodi huo kwa mujibu wa sheria. 

“Mgodi huu unahatarisha maisha ya watu japo nafahamu unaleta fedha kwa Serikali na kutoa ajira, lakini ninyi wawekezaji hamtendi haki kwa wananchi wa kawaida na ukiangalia mazao yanalimwa kule bondeni kama kuna heavy metal (kemikali) maana yake inakwenda kuathiri afya za wananchi.

“Watu wangu (NEMC) walitoa maelekezo mrekebishe hizi changamoto za kimazingira tangu tarehe tano mwezi wa nane maana yeke tarehe tano mwezi wa kumi na moja mlitakiwa muwe mmerekebisha lakini bahati mbaya mpaka leo hii marekebisho, mnafanya kosa juu ya kosa,” alifafanua.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Ziwa kutoka Baraza hilo, Bw. Jarome Kayombo alisema wamepokea maelekezo ya Waziri na kuahidi kuchukua sampuli za maji yanayotiririka ili kubaini ni kwa kiasi gani uchafuzi huo unafanyika.

Alisema baada ya kubaini mapungufu hayo waliwapa onyo kwa kuwapiga faini ya sh. milioni lakini hadi Novemba mwaka huu wameonekana bado hawajatekeleza hivyo watashauriana na mwanasheria wa Baraza kuona ni hatua gani za kuchukua dhidi ya mwekezaji huyo.

Aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana na wawekezaji wakiwemo wenhe migodi ya dhahabu kwa kutoa ushauri wa kitaalamu kimazingira kwa kuwa NEMC haiku kwa ajili ya kutoa adhabu bali kuwasaidia ili wafuate sheria. 

Nae Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Sinyamule aliomba NEMC kuwashirikisha katika shughuli za ukaguzi wa migodi ikiwemo kuwapatia ripoti ili wawe wanafuatilia maelekezo endapo yanatekelezwa ama la.

Alisema uongozi wa mkoa utaendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais katika kuhakikisha maelekezo ya Serikali kuhusu suala zima la usimamizi wa mazingira yanatekelezwa ili kulinda afya za wananchi. 

Nae Mtaalamu wa mazingira wa mgodi huo, Bw. Francis Sirili aliahidi kuwa watafuata maelekezo yaliyotolewa na Serikali kwa kuzifanyia kazi changamoto zilizobainishwa.

Share To:

Post A Comment: