Thursday, 18 November 2021

Waziri Ummy aahidi usimamizi wa afua za lishe katika Mamlaka za Serikali za Mitaa

 


Na. Angela Msimbira TANGA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu  amesema  Ofisi ya Rais –TAMISEMI itasimamia kikamilifu  utekelezaji wa afua za Lishe kwenye Sekretarieti za Mikoa na Malaka za Serikali za Mitaa.


Akiongea leo katika Mkutano  Mkuu wa saba wa Wadau wa masuala ya lishe  nchini uliofanyika Jijini Tanga  Waziri Ummy amesema   Ofisi ya Rais - TAMISEMI inaahidi  kusimamia utekelezaji wa mpango  wa afua za lishe kwa kutenga  kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto chini ya miaka mitano, lengo ni kupunguza udumavu wa ukuaji wa watoto katika jamii  kwa kuimarisha lishe bora  nchini.


Waziri Ummy anaendelea kufafanua  kuwa fedha hizo zitatengwa katika fungu la maendeleo  kwa kuwa katika mkakati wa kuimarisha lishe nchni  ofisi ya Rais - TAMISEMI inatakiwa  kuchangia  asilimia 10.5  sawa na kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 67.2 kwa miaka mitano, hivyo suala hilo litatekelezwa kikamilifu.


Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itasimamia fedha zilizopangwa kwa ajili ya shughuli za lishe kwenye Halmashauri zote 184  nchini  na kutoa taarifa za mapato na matumizi ya Halmashauri kwa mwaka ikiwemo asilimia kumi  kwa ajili ya mikopo ya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu.


Amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI  itahakikisha fedha ambazo zimetengwa kwenda kutatua afua za lishei zinatumika kama zilivyoelekezwa na kuhakikisha inazibana  Halmashauri ambazo hazijatoa fedha hizo kwa wakati.


Amesema itaendelea  kusimamia  utendaji wa afua za lishe katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kufanya tathmini  ya mikataba ya lishe iliosainiwa na Wakuu wa Mikoa kote nchini  kuanzia ngazi ya Kitaifa, Mikoa, Vijiji, Kata na vitongoji na kuhakikisha na kuimarisha uwajibikaji kwa viongozi na watendaji wa  ngazi zote.


Waziri Ummy amesema Ofisi ya Rais - TAMISEMI itasimamia utoaji wa taarifa  zenye ubora na wakati kuhusu afua za lishe kwa wakati kupitia mfumo wa utoaji wa taarifa wa  intergreted  monitoring and  evaluation system unaosimamiwa na Ofisi ya  Rais - TAMISEMI kwa kipindi cha  robo mwaka na taarifa hizo zitatumwa kwenye mfumo wa National multsectrol  Management Information system unaosimamiwa na taasisi ya chakula na lishe  kwa ajili ya kupata taarifa kitaifa.


Aidha, amesema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua  kali za kinidhamu  viongozi au maafisa  waliochini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa uzembe wa utekelezaji  na matumizi mabaya ya fedha za lishe zitakazobainishwa.

No comments:

Post a Comment