Thursday, 25 November 2021

EAC yazindua Kampeni ya Utalii kutangaza utalii wa EAC

 


Na Jane Edward, Arusha


Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Dkt Peter Mathuki amezindua rasmi Kampeni ya Vyombo vya Habari vya Utalii wa Kikanda Ndani ya Jumuiya hiyo inayolenga kutangaza bidhaa na huduma za utalii za kitaifa na kikanda, hatua inayotajwa ni kuchochea safari za ndani ya kanda.


Mathuki ameyasema hayo Jijini Arusha wakati wa kuzindua kampeni hiyo iliyopewa jina la 'Tembea Nyumbani'.


Amesema kuwa lengo ni kushawishi waafrika Mashariki kusafiri katika nchi zao katika jitihada za kufufua Utalii wa ndani katika ukanda huu wa Afrika mashariki.Aidha amesema kampeni hiyo imepangwa kuendeshwa kwa wiki tatu, kuanzia tarehe 1 Desemba, 2021 huku ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Uuzaji wa Utalii wa jumuiya na Mpango wa Kufufua EAC unaoungwa mkono na Shirika la Maendeleo la Ujerumani, GIZ.


Akifafanua zaidi Mathuki amesema utalii unachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Nchi Wanachama wa jumuiya hiyo na kabla ya janga la uviko 19,  utalii ulichangia 10% ya Pato la Taifa (GDP), 17% mapato ya nje na 7% katika uzalishaji wa ajira.


"janga la COVID-19 lilishuhudia sekta ya utalii ikiathiriwa vibaya huku watalii wa kimataifa wanaofika Afrika Mashariki wakipungua kwa takriban 67.7%, hadi wastani wa waliofika milioni 2.25 mwaka 2020 ikilinganishwa na milioni 6.98 mwaka 2019"Alisema Dkt Mathuki.


Hata hivyo Kampeni hiyo ya Tembea Nyumbani inafanywa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Jukwaa la Utalii la Afrika Mashariki linalowakilisha biashara za utalii katika kanda nzima.


Kupitia kampeni hiyo, wamiliki wa hoteli na watoa huduma wengine wa utalii wametakiwa kutangaza vifurushi vya bei nafuu kwa wananchi wa EAC ili kuweza kujitangaza zaidi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa EAC anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji, BwJean Baptiste Havugimana amebainisha kuwa EAC inapiga hatua katika kuhakikisha Visa ya Utalii Moja inapitishwa na Nchi Wanachama wa EAC.


“Baraza la Kisekta la Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori katika kikao chao cha kilichofanyika tarehe 15 Julai 2021 ilipendekeza Sekretarieti iitishe mkutano wa sekta mbalimbali unaojumuisha sekta muhimu kama vile Utalii na Wanyamapori, Uhamiaji na Usalama ili kuandaa mfumo wa utekelezaji kuanzishwa kwa Visa Moja ya Utalii na Nchi Wanachama,” alisema.

No comments:

Post a Comment