Sunday, 10 October 2021

WAZIRI MHAGAMA AGUSWA NA UTENDAJI WA NSSF KWA KUTOA MSAMAHA WA TOZO KWA WAAJIRI WENYE MALIMBIKIZO YA MICHANGO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, akipata maelezo kuhusu mradi wa shamba la miwa Kagera kutoka kwa Mhandisi Francisco Sikalumbi wakati alipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha sukari Kagera mwishoni mwa wiki. Kushoto ni mwekezaji wa kiwanda hicho Seif Seif.

Mwekezaji wa kiwanda cha sukari cha Kagera, Seif Seif akimuonesha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (kulia), namna wanavyotumia maji kutoka Mto Kagera kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji wa miwa katika kiwanda hicho, wakati wa ziara ya Waziri Jenista katika kiwanda hicho mwishoni mwa wiki. 


Na Mwandishi Wetu, Kagera

 SERIKALI kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, imewaomba waajiri wote nchini, kutumia fursa adhimu iliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ya kutoa msamaha kwa waajiri wote wenye malimbikizo ya tozo zitokanazo na ucheleweshaji wa michango.

Waziri Mhagama alisema hayo mwishoni mwa wiki alipotembelea kiwanda cha sukari Kagera kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa pamoja na kuangalia shughuli za NSSF zinazofanywa kiwandani hapo ikiwemo uwasilishwaji wa michango

Alisema msamaha huo umeanza tarehe 1 Oktoba, mwaka huu na unahusu waajiri wote wenye malimbikizo ya michango na tozo kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2021 kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.

“Niwaombe waajiri watumie hii fursa iliyotolewa na NSSF kwani huu ni utekelezaji wa maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kila siku anatafuta mbinu ambazo zitarahisisha shughuli za uwekezaji nchini,” alisema.

Waziri Mhagama alisema waajiri watakaolipa malimbikizo ya michango kuanzia mwezi huu Oktoba 2021 mpaka tarehe 31 Novemba, 2021 watalipa msamaha wa tozo zitokanazo na ucheleweshaji wa michango husika kwa kiwango cha asilimia 100 jambo ambalo ni fursa kubwa kwa waajiri hao.

Alisema waajiri watakaolipa malimbikizo ya michango ifikapo tarehe 31 Disemba, 2021 watapa msamaha wa tozo zitokanazo na ucheleweshaji wa michango husika kwa asilimia 75 na waajiri watakaolipa malimbikizo ya michango ifikapo tarehe 31 Januari, 2022 watapata msamaha wa tozo kwa kiwango cha asilimia 50

“Niwaombe sana wawekezaji wote, waajiri wote nendeni mkashirikiane na NSSF kwenye ofa hii ambayo katika Mfuko  tumeweza kupata msamaha huu hivyo tuitumie vizuri nafasi hii,” alisema. 

Aliishukuru NSSF kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanachama na wadau ili kuhakikisha wanapata huduma nzuri, ambapo alitoa wito kwa waajiri wengine wote waliopo kwenye sekta binafsi kuhakikisha wanajisajili na kuwasajili wafanyakazi wao pamoja na kuwapelekea michango yao NSSF kwa wakati kwani hilo ni takwa la kisheria.

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora aliupongeza Mfuko wa NSSF katika mkoa huo kwa kuweza kupunguza kero za wanachama na wadau kwa asilimia zaidi ya 90 kutokana na muda mrefu sasa uongozi wa mkoa huo haujapokea malalamiko yoyote ya wanachama wa NSSF.

Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Cosmas Sasi akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Mshomba, alisema kiwanda cha sukari cha Kagera kwa upande wa NSSF ni mdau mkubwa kwani kina wanachama 8,000 ambao wanachangia kila mwezi takribani Shilingi milioni 540.

Aidha, Mbunge wa Nkenge, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Mhe. Florent Kyambo, alisema mwekezaji huyo licha ya kutengeneza ajira kwa Watanzania, lakini ni mlipaji mzuri wa michango ya wafanyakazi wake NSSF.

Naye, mwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Kagera, Seif Seif alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kuwa na dira ya kukuza viwanda vya ndani na kuweza kuvilinda ili viweze kukua.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Mhandisi Atugonza Phinis ambaye ni mwendeshaji mitambo kiwandani hapo, alisema kampuni ya Kagera imekuwa ikitoa ajira nyingi kwa vijana na kwamba wanafurahishwa na namna mwekezaji huyo anavyojali maslahi ya wafanyakazi wake kwa kuwasilisha michango NSSF ili pale watakapopatwa na janga waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na mfuko huo.


No comments:

Post a Comment