Monday, 18 October 2021

Kilindi yafikia asilimia 99.1 ya unyonyeshaji watoto wenye mwezi 0 hadi miezi sita


Raisa Said, Kilindi

Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga  imefanikiwa kufikia asilimia 99.1  ya unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa mwaka  2020/21 kwa watoto wa miezi 0 hadi miezi 6 kutokana na jitihada za idara ya Afya  kuendelea kutoa elimu ya unyonyeshaji kwa jamii.


Akizungumza na Waandishi wa habari  Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dk Daniel Chochole amesema miaka ya nyuma wilaya hiyo ilikuwa na kiwango cha chini cha unyonyeshaji  ukilinganisha na kipindi hiki.

Dk Chochole alisema kuwa  moja wapo ya afua wanazotekeleza ni kuhamasisha  unyonyeshaji kwa watoto wanaozaliwa tangu umri 0 hadi miezi sita  sababu maziwa ya mama yanavirutubisho vya kutosha."Usimwage maziwa ya kwanza ya mama baada ya kuzaa, huwa na protini na kingamwili ambayo ni muhimu kwa mtoto mchanga. Unapaswa kumpa mtoto mchanga, kwa sababu ni ‘chanjo’ ya kwanza ambayo mtoto atapata.


Mwanakombo Jumaa Mkazi wa barabara ya 20 mwenye mtoto wa miezi mitatu alisema ,anatambua umuhimu wa elimu wanayopewa na watoa huduma wa Afya  toka mama akiwa mjamzito hadi kujifungua kuhusu suala la unyonyeshaji.


“Kliniki ya kwanza tu nikiwa na mme wangu tuliambia baada ya kujifungua mtoto anatakiwa anyonyeshwe maziwa ya mama pekee hadi atakapofikisha miezi sita."Alisema Mwanakombo  ambaye ni Mama mwenye watoto sita.


Kwa mujibu wa Mwongozo wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto kuhusu maadhimisho ya wiki ya unonyeshaji Tanzania imepiga hatua katika unyonyeshaji wa maziwa ya mama ambapo idadi ya wanawake asilimia 98 wanachagua kuwanyonyesha watoto wao.


Asilimia 53.5 ya watoto wanaanzishiwa kunyonya maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.


Pia  takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 58 ya watoto wananyonyeshwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa ,Watoto wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia umri wa mwaka mmoja ni asilimia 92.2 huku wanaoendelea kunyonyeshwa hadi kufikia miaka miwili ni asilimia 43.

 

No comments:

Post a Comment