Na Mwandishi wetu


ONESHO la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki  [East Africa Regional Tourism Expo-EARTE 2021] linalotarajiwa kufanyika viwanja vya Tanganyika Game Trackers [TGT], Arusha linatarajiwa kuwa na Mawaziri wa Utalii zaidi ya 18 kutoka nchi za Afrika. 


Akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo 6 Oktoba, Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro alisema kuwa,  Tanzania imekuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza  wa onesho hilo ambapo imevutia viongozi wengi wa sekta hiyo Afrika.


"Mpaka sasa nchi zote za Afrika Mashariki zimethibitisha ushiriki wake. Kwa hiyo kutakuwa na nchi sita na kila nchi zitakuja na Mawaziri wake, viongozi wake wa Serikali na sekta binafsi wa huduma za kitalii.


Pia Mawaziri wengine 12 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika wamethibitisha kushiriki" Alisema Waziri Dkt. Damas Ndumbaro  na kufanya idadi ya Mawaziri wa Utalii  kufikia 18.


Wadau wengine waliothibitisha kushiriki ni Afrika Tourism Board ambao wamependa kutumia tukio hilo kutoa tuzo kwa viongozi mbalimbali ambao wamefanya vizuri katika sekta ya utalii barani Afrika na wengine ni UNWTO taasisi ya Umoja wa mataifa nayo imethibitisha kushiriki licha ya kuandaliwa kqa muda mfupi limepata muitikio mkubwa sana". Alisema Waziri Dkt. Ndumbaro.

 

Ambapo pia alitoa rai kwa Waandishi wa habari kuwepo kwenye onesho hilo kwa wingi ili waijuze dunia nini kinaendelea Tanzania sambamba na kuwaomba wadau wa Utalii  kwani ushiriki wao ni muhimu sana kwenye  onesho hilo la kihistoria.


"Hii ni historia kwa mara kwanza hapa nchini kwetu, sisi kama wizara tumejipanga na tutaendelea kujipanga na kuhakikisha kwamba matukio makubwa kama haya yanaendelea kuja  Tanzania pili kuleta utalii wa mikutano na utalii mwingine ambao tunazani ni muhimu sana.


Katika uzinduzi rasmi hiyo 9 Oktoba tunamtarajia kuwa na kiongozi mkubwa wa Nchi ambapo sambamba na hilo kutakuwa na maonesho ya siku tatu 9-11 Oktoba ndani ya viwanja na 12-16 kutakuwa na na safari za kiutalii wadau wote wanakaribishwa kushiriki wakiwemo Wanahabari, Tour Operator na Wananchi wote.


Aidha, Waziri Dkt. Ndumbaro amefuta tozo za kuingilia kwenye maeneo yote ya Utalii nchini ikiwemo maeneo ya Hifadhi kwa muda wa wiki moja kuanzia 9-16 Oktoba mwaka huu kwa watu watakaojiandikisha kwenye 

onesho  hilo  katika  viwanja vya Tanganyika Game Trackers [TGT], Arusha.


"Katika kuunga mkono juhudi za kuitangaza Utalii wa Tanzania na kuunga mkono Royal Tour ambayo Mhe Rais wa awamu ya sita,  Samia Suluhu Hassan alianzisha, wizara imefuta tozo  ‘Park fee’ kwa muda wa wiki moja wakati wa ‘tours zote za wanaoshiriki na kujiandikisha kwenye  onesho.

 

Hii ni kwa wale waliojisajili na kupata namba ya mshiriki na kwa kutumia namba hiyo ya usajili unaweza kwenda ‘National Park’ yoyote kwa muda  huo wa wiki moja ukatembea pasipokulipia tena malipo hayo  ila utakacholipa ni usafiri ambao utakodi kwa kampuni binafsi na pale utakapolala kwa sababu serikali hatuna mamlaka kwa sehemu za watu binafsi, lakini zile tozo za Serikali kwa muda wa siku saba zote tunazisimamisha  ili onesho letu la kwanza lipewe heshima ambayo inastahili.


"Wenzetu Afrika Mashariki wametupa heshima Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuandaa onesho hilo na baada ya hapo kila mwaka itakua inaenda kwenye nchi nyingine ikianza na Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan Kusini na baadae kurudi tena Tanzania" alisema Waziri Dkt. Ndumbaro.

 

Ambapo ameongeza kuwa, hiyo ni heshima kubwa kwa Tanzania kuweza kuandaa onesho kwa muda Wa wiki nzima kwani manufaa yake ni makubwa sana  na kupitia onesho hilo, wanunuzi na wauzaji wa huduma za  kitalii wanakutana wa ndani na nje ya nchi.


Waziri Dkt. Ndumbaro amewapongeza wadhamini waliojitokeza kudhamini onesho hilo wakiwemo; Benki za CRDB, NMB, Pia wapo chama cha wamiliki watalii Tanzania [TATO], TBC, ITV, TANAPA na wengine wengi.


Onesho hilo linaratibiwa na Bodi ya Utalii [TTB], kwa kushirikiana na  Taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar (ZCT) pamoja na wadau wengine wa Utalii.

Tanzania imepewa dhamana ya kuratibu onesho  ambapo linatengemea kuwa na Mawakala wa utalii yaani "Hosted Buyers" kutoka nchi mbalimbali duniani, wadau wa utalii kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Africa Mashariki na kampuni za Tanzania zinazotoa huduma za malazi, chakula na usafiri kwa watalii za Tanzania, Pia kutakuwa na wadau/wajasiliamali wanaohusika na kuuza vitu mbalimbali vinavyotengenezwa kwa malighafi zinazopatikana nchini Tanzania.

 

Aidha  TTB, imeweka gharama rafiki za kiingilia katika maonesho hayo ambapo kiingilio kwa mtu mzima ni shilingi 10,000 na mototo shilingi  5,000 na kwa siku ya jumapili imepangwa kuwa siku ya familia hivyo kutakuwa na kiingilio maalumu ya shilingi 20,000 kwa ajili ya familia.

Share To:

Post A Comment: