Na Joseph Lyimo

JAMII za kifugaji ambazo kwa asilimia kubwa wanaishi mikoa ya kanda ya kaskazini bado kuna baadhi ya mila na desturi zinamkandamiza mtoto wa kike ikiwemo ndoa za utotoni na kuwakosesha elimu.

Mwanafunzi wa darasa la sita katika moja ya shule ya msingi iliyopo Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Esupati Mollel (siyo jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 14 anaelezea namna alivyoishi kwa miaka mitatu shuleni akisoma huku akiwa mchumba wa mzee wa miaka 70.

Esupati anasema kwa muda wote huo wa miaka mitatu tangu akiwa darasa la nne mwaka 2019 na sasa yupo darasa la sita amekuwa akidhihakiwa na baadhi ya wanafunzi wenzake kuwa yeye ni mchumba wa watu anayesubiria kuolewa.

Amesema hali hiyo imejitokeza baada ya wanafunzi wenzake kubaini kuwa amechumbiwa na mzee na anasubiriwa kuolewa tangu mwaka 2019 akiwa darasa la nne.

Anasema wanafunzi wenzake huwa wanamcheka kutokana na yeye kulipiwa mahari ya ng'ombe 10 na anasubiri kuolewa pindi akihitimu darasa la saba mwaka kesho 2022.

"Huwa wanasema wewe utatueleza nini wakati umeshachumbiwa na unasubiri kuolewa na mzee wa miaka 70 mara baada ya kumaliza darasa la saba hivyo nakwazika nafsini mwangu," amesema Esupati.

Amesema mara kwa mara amekuwa akizomewa na wanafunzi wenzake darasani ila hana chakufanya kwani wazazi wake ndiyo wamesababisha hali hiyo kwa kuchukua ng’ombe 10 hivyo yeye kuchumbiwa.

“Nilikuwa na ndoto za kuwa mwalimu pindi nikihitimu masomo yangu, kwani nitafaulu na kwenda sekondari nikijaliwa uzima baada ya kufanya mtihani wa darasa la saba,” amesema Esupati.

Amesema hata hivyo, ndoto hizo zitakwamishwa kutokana na yeye kusubiri kuolewa mara baada ya kumaliza kufanya mtihani wa darasa la saba mwakani.

Diwani wa kata ya Shambarai, Julius Lendauwo amesema changamoto za baadhi ya wazazi kutaka kuwaozesha mabinti zao bado zipo ila serikali imekuwa ikikemea hilo.

“Tumekuwa tukiwaeleza wafugaji kuwa tunapaswa kubadilika kwa kuwaacha watoto wetu wasome na tusiwaozeshe wala kuwalazimisha kuchunga mifugo wangali wadogo,” amesema.

Hata hivyo, Kaimu katibu tawala wa Wilaya ya Simanjiro, Mussa Waziri akizungumza mji mdogo wa Mirerani na jamii ya wafugaji wa eneo hilo amesema serikali itasimama kidete kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu.

Mussa amesema serikali ya wilaya hiyo inaahidi kuwa wanafunzi wote walioandikishwa watasoma na kumaliza elimu zao na watasimamia hilo.

Amesema serikali itawachukulia hatua kali za kisheria wazazi na walezi ambao watashiriki kuwakwamisha watoto wao kusoma ikiwemo kuwaozesha wakiwa wadogo au kuwapa kazi ya kuchunga mifugo
Share To:

Post A Comment: