Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi
Liberata Mulamula (Mb) ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa
Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Commission for
Cooperation-JCC) kati ya Tanzania na Kenya unaofanyika jijini Nairobi,
Kenya kuanzia tarehe 19 hadi 24 Agosti, 2021.
Akiwa nchini Kenya,
Mhe. Balozi Mulamula anatarajiwa kukutana kwa mazungumzo na Mwenyeji
wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Mhe. Balozi Raychelle Omamo tarehe
23 Agosti 2021 pamoja na kutembelea Chuo cha Ulinzi cha Taifa cha Kenya
ambapo atatoa mhadhara kwa mada isemayo “Mtazamo wa Tanzania kwenye
Agenda ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama”.
Mkutano
huu ulioanza katika ngazi ya wataalam tarehe 19 hadi 22 Agosti 2021,
umeongozwa na Balozi Naimi Aziz, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki huku upande wa
Kenya ukiongozwa na Balozi George Orina, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika
na Umoja wa Afrika.
Pamoja na mambo mengine Mkutano wa Wataalam
umejadili agenda mbalimbali za ushirikiano ambazo zitawasilishwa kwenye
kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika tarehe 23 Agosti 2021 kabla ya
Mkutano wa Nne wa Tume ya Ushirikiano kuhitimishwa na Mkutano wa
Mawaziri tarehe 24 Agosti 2021.
Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja
ya Ushirikiano utashuhudia uwekwaji saini wa hati tatu (3) za
makubaliano (Memorundum of Understanding – MoU) ambazo ni; Hati ya
Makubaliano ya Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia. Kusainiwa kwa
kwa makubaliano haya kutaendeleza na kuimarisha mahusiano mazuri ya
kisiasa na kidiplomasia yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya.
Hati nyingine itakayosainiwa ni kuhusu Uhakiki wa Mpaka kati ya Tanzani
na Kenya. Kusainiwa kwa Hati hiyo kutazipa Nchi zote mbili msingi wa
kisheria wa kuhakiki mpaka uliowekwa na wakoloni kwa kuuimarisha na
kuweka alama zinazoonekana ili kuondoa mwingiliano wa jamii za mpakani
na hivyo kupunguza migogoro ya mara kwa mara.
Mwisho ni Hati ya
Makubaliano ya Ushirikiano katika Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.
Hati hii inalenga kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi za pande zote
katika maeneo ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ili kuleta manufaa
kwa nchi zote katika kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa masuala ya
elimu ya juu, Sayansi na teknolojia kwa pande zote.
Tanzania na
Kenya zimeendelea kutekeleza masuala mbalimbali ya ushirikiano katika
sekta za biashara, uwekezaji, siasa na diplomasia, elimu, uhamiaji,
utalii, kazi, afya, usafirishaji, ulinzi na usalama.
Tume ya
Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ilianzishwa rasmi mwezi
Septemba 2009 jijini Arusha, Tanzania na kufuatiwa na Mkutano wa Kwanza
wa Tume hiyo uliofanyika jijini hapo mwaka 2009. Mkutano wa Pili wa Tume
hiyo ulifanyika jijini Nairobi, Kenya mwezi Septemba 2012 na Mkutano wa
Tatu ulifanyika jijini Dar es Salaam mwezi Desemba 2016.
Mkutano
wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya
unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Mhe. Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru
Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walipokutana wakati wa ziara ya Mhe.
Rais Samia iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.
Home
Unlabelled
WAZIRI MULAMULA KUONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA NNE WA TUME YA PAMOJA YA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA KENYA.
Post A Comment: