SERIKALI Wilaya ya Kibaha ,imemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha na idara ya afya ,kuhakikisha zahanati kata ya Mkuza ianze kazi ili kuondoa changamoto ya baadhi ya wakazi kufuata huduma za afya Mwendapole kwa umbali wa km.20.


Kata hiyo inatajwa kuwa na kaya 3,613 na idadi ya watu 25,121 ambao walikuwa na changamoto ya miaka mingi kukosa kituo cha afya ama zahanati ya serikali .

Akitoa agizo hilo ,katika ziara ya kamati ya siasa ya CCM Kibaha Mjini ,ilipotembelea mradi wa zahanati hiyo ,mkuu wa Wilaya ya Kibaha ,Sara Msafiri alisema amejiridhisha na kamati hiyo kukamilika kwa jengo na kuwepo na vifaa vya kuanza huduma za awali.

"Tumekiridhisha na kamati ya siasa niliyoambatana nayo ,awali kulikuwa na mgogoro wa Ardhi umeisha ,changamoto bado kibali kwa ajili ya utekelezaji "

"Lakini hapa pia kuna idadi kubwa ya wananchi ni busara kuanza utekelezaji mara moja wakati taratibu nyingine zikiendelea "anasema Msafiri.

"Serikali inaendelea kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi ili kuwapunguzia kero sugu ya kutembea kufuata huduma za afya mbali hali inayosababisha usumbufu na wakati mwingine wajawazito na watoto kupata tabu"Alifafanua mkuu huyo wa Wilaya.

Msafiri alimuelekeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,kufanya ukaguzi katika vituo vya afya vyenye vifaa vya ziada ili vipelekwe hapo na wataalam wa afya .

Nae mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid Bundala alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na ile ya kimkakati .

Aliunga mkono agizo hilo la mkuu wa Wilaya na kuongeza ,litakwenda kunufaisha wakazi wa Bungo,Mkuza,Mpakani,Mbwate,Mkongoni na Kibondeni .

Awali ofisa mtendaji kata ,Enea Hezron alieleza ,Ujenzi huo ulianza 2015 na kufikia 2021 umekamilika kwa gharama ya milioni 274,477,470.

Mkazi wa eneo hilo ,Asha Athumani alisema ,wakazi wa Bungo walifuata huduma za afya Mwendapole kwenye urefu zaidi ya km.20.

Aliipongeza serikali kutatua kero za kiafya na kuboresha huduma za afya kwa kusogeza huduma karibu na jamii.

Kamati hiyo ya siasa Kibaha Mjini,imetembelea baadhi ya miradi ya elimu ,afya,soko,machinjio katika kata ya Mbwawa ,Misugusugu ,Mkuza ,Viziwaziwa na Pangani .
Share To:

Post A Comment: