Friday, 27 August 2021

70% YA WATOTO CHINI YA MIAKA 5 HAWANYONYESHWI IPASAVYO

Mama akimnyonyesha mwanae huku akili na mawazo yake yote yakiwa kwa huyo mwanae kuonesha upendo na kumjali.
Mtoto akifurahia ziwa pamoja na mapenzi ya karibu ya mama yake.
Ofisa Lishe Mkoa wa Singida Teda Sinde akifafanua jambo kuhusiana na suala zima la unyonyeshaji
 


Na Abby Nkungu, Singida 

ZAIDI ya asilimia 70 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano mkoani Singida,  huwa hawanyonyeshwi  maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya, hali inayoathiri afya zao, malezi, makuzi  na usalama wa kundi hilo katika jamii.

Takwimu kutoka Idara ya lishe mkoa wa Singida zimekuja wakati huu ambapo Dunia inaadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji maziwa ya Mama ili kulinda afya na kuimarisha kinga ya watoto.

Utafiti wa Kitaifa wa mwaka 2018/19 juu ya Hali ya lishe mkoani Singida, unaonesha asilimia 27.9 ya watoto wa chini ya miaka mitano ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia 3 tu ya watoto walio na umri wa chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora.

"Hii ndio sababu kubwa ya watoto wengi  kuwa na matatizo ya lishe na kiafya ambapo hali halisi inaonesha asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo" alisema Ofisa Lishe Mkoa wa Singida, Teda Sinde.

Alisema kuwa matatizo hayo yametokana na familia nyingi kuacha kuzingatia suala la Uzazi wa Mpango; hivyo kujikuta wakizaa mtoto mwingine kabla ya yule wa awali kutimiza miaka miwili.

Alieleza kuwa jambo hilo husababisha mtoto wa awali kuachishwa kunyonya; hivyo kuathiri afya, malezi, makuzi, usalama na matunzo kwa mtoto aliyetangulia kwa kuwa mzazi au mlezi hulazimika kuhamishia mapenzi kwa mtoto mchanga aliyezaliwa.

Dk Suleiman Muttani  ambaye  ni Daktari Bingwa  mshauri  wa magonjwa ya wanawake na watoto katika  hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida,  alieleza kuwa mtoto kutonyonyeshwa maziwa ya mama kwa miaka isiyopungua miwili kama inavyoshauriwa, hupata athari mbaya  za kiafya.

"Baadhi ya athari hizo ni pamoja na ukuaji duni wa ubongo hivyo kusababisha mtoto kutofundishika kirahisi na kuwa mzito kwenye kufikiria na kutoa maamuzi, husababisha upungufu wa damu mwilini, huathiri mfumo wa kinga ya mwili kwa ajili ya kupambana na magonjwa na kupata utapiamlo na magonjwa mengine ambayo yanaweza kusababisha vifo" alisema.

Hata hivyo, baadhi ya akinamama; akiwemo Agatha Majoya na  Nyagili Soteri wanasema kuwa tatizo  kubwa ni elimu duni juu ya umuhimu  wa Uzazi  wa Mpango huku Hamoud Hafidh na Ali Alute wakidai kuwa imani potofu juu ya baadhi ya njia kuwa na madhara ya kiafya, ni changamoto nyingine.

Mwito wao ni kwa Waatalamu wa afya, maofisa lishe na  wadau wengine kuendelea kutoa  elimu juu ya  umuhimu  wa Uzazi wa mpango na  kukemea mila potofu ili kuhakikisha kila mtoto anapata kikamilifu haki ya maziwa ya mama kama inavyoshauriwa na Wataalam wa afya. 

No comments:

Post a Comment