Naibu Waziri Wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) akisisitiza kwa wakandarasi kukamilisha kwa wakati mradi wa usambazaji maji wa B2F kutoka Chuo Kikuu hadi Bagamoyo Wenye thamani ya Bilion 65.
Naibu Waziri Wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akipanda juu kukagua ujenzi wa mradi wa maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). Maryprisca amesisitiza wakandarasi kukamilisha kwa wakati mradi wa usambazaji maji wa B2F kutoka Chuo Kikuu hadi Bagamoyo Wenye thamani ya Bilion 65.
Moja ya tanki la ujazo wa Lita Milioni tano katika mradi wa usambazaji maji wa B2F kutokea Chuo Kikuu hadi Bagamoyo linalojengwa katika eneo la Tegeta A.
 

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka wakandarasi wa mradi wa uboreshaji maji kutola Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo  kukamilika ndani ya wakati.

Mradi huo wa uboreshaji maji kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa thamani ya Bilioni 65 ikiwa ni fedha za mkopp kutoka Benki ya Dunia.

Akizungumza wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kutembelea miradi inayotekelezwa na DAWASA, Naibu Waziri amesema mradi wa uboreshaji maji ni moja ya  miradi mikubwa inayotekelezwa kimkakati inayoenda kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Maryprisca amesema, Wizara bado inaendelea kuboresha huduma za maji kwa wananchi na kukamilila kwa mradi huo kutasaidia kufanya maunganisho mapya elfu sitini (60,000).

“Huu mradi wa Kutokea Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo utakapokamilika utafanya maunganisho mapya elfu sitini (60,000) na hii haitakuwa mwisho serikali tutaendelea kuboresha huduma kwa kuleta miradi mipya,”amesema

“Kukamilika kwa mradi huu kutaenda kuondoa kero ya maji kwa wananchi hata wale wa Goba ambao wamekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu  na ujenzi wa matanki haya matatu utaenda kuondoa tatizo la maji sambamba na mgao,” amesema

Mheshimiwa Maryprisca amesisitiza kwa wakandarasi watakaoshindwa kukamilisha miradi kwa wakati kuwa serikali haitawafumbia macho na itawachukulia hatua ikiwemo kuvunja mikataba ili kulinda maslahi ya watanzania.

“Sisi hatutaki wakandarasi wajanja wajanja katika kutekeleza miradi yetu na hatutasita kuvunja mkataba tukiona mkandarasi anashindwa kutekeleza makubaliano kwa wakati na hilo limeweza kutokea pia katika mradi wa Same-Mwanga na Waziri Jumaa Aweso aliweza kuvunja mkataba nao,” amesema Mheshimiwa Maryprisca.

Aidha, amesema katika kutekeleza miradi mikubwa kama hii kunajitokeza changamoto mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa msamaha wa kodi ila amewahakikishia wakandarasi kuwa Wizara yake imeliona hilo na limeshalifanyia kazi.

Mheshimiwa Maryprisca amewapongeza wananchi waliokubali maeneo yao kupita kwa mradi huo ambao utaondoa kero ya maji.

Naye Mkurugenzi wa Miradi na Uwekezaji DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema mradi huu umeanza ujenzi mwaka 2019 na unatarajia kukamilika ndani ya miezi 24 ambapo mwishoni mwa mwaka huu mkandarasi anatakiwa kukabidhi mradi huo.

Mtindasi amesema watajenga matanki makubwa ya Lita Milioni 5 pia watajenga vituo vya kusukumia maji (Booster station) na kulaza mabomba kwa umbali wa Kilomita 1000.

“Tunatekeleza mradi huu kwa fedha tulizofadhiliwa na Benki ya Dunia kiasi cha Bilioni 65 ambapo tutajenga matanki makubwa, vituo vya kusukumia maji (booster station)na ulazaji wa mabomba na utaenda kutoa huduma kwa wateja elfu sitini (60,000) kuanzia Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo,” amesema Mhandisi Mtindasi.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa matanki matatu yenye ujazo wa Lita Milioni 5, vituo vya kusukumia maji vikubwa viwili (booster station) na italaza mabomba kwa umbali wa Kilomita 1000 kuanzia Chuo Kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo na utaweza kuunganisha wateja wapya 60,000.
 
Share To:

Post A Comment: