Wednesday, 21 July 2021

TIMU ZINAZOSHIRIKI LIGI YA NETIBOLI ZATAKIWA KUTUMIA VIPAJI KUTOKA

 
Mshambuliaji wa pembeni wa timu ya netiboli ya Uhamiaji ya Dar es salaam Fatuma Chenge akijaribu kufunga mojawapo ya magoli ambapo Magereza walishinda kwa magoli 37-36.
Mshambuliaji wa pembeni wa timu ya netiboli ya Magereza Morogoro Naima Boli akijaribu kufunga mojawapo ya magoli ambapo Magereza walishinda kwa magoli 37-36
Afisa Michezo wa Jiji la Arusha Benson Maneno akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa ligi ya netiboli katika uwanja wa sheikh Amri Abeid jijini Arusha
Katibu Mkuu wa CHANETA Judith Ilunda akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa ligi ya netiboli katika uwanja wa sheikh Amri Abeid jijini Arusha

……………………………………………………………………

Na Mathew Kwembe, Arusha

Timu zinazoshiriki mashindano ya ligi daraja la kwanza netiboli zimetakiwa kuwatumia wachezaji wenye vipaji kutoka katika michezo ya UMISSETA ili kuwawezesha wachezaji hao kukuza vipaji vyao lakini pia kuondokana na mtindo wa kila mwaka kutegemea wachezaji hao hao.

Kauli hiyo imetolewa jana jijini Arusha na Afisa Michezo wa Jiji hilo Benson Maneno mara baada ya ufunguzi wa mashindano ya ligi ya netiboli uliofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Amesema kuwa wao kama jiji la Arusha wameutumia mfumo huo ambapo wameweza kuchukua wachezaji wengi waliowahi kushiriki michezo Michezo ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) ambayo ilimazika hivi karibuni mjini Mtwara.

Sambamba na hilo, Maneno amewataka waandaaji wa ligi ya netiboli ambao ni CHANETA kuhakikisha kuwa mashindano haya yasiwe yanafanyika mwezi wa saba kwani taasisi nyingi za serikali zinashindwa kuleta timu.

“ Ni kipindi ambacho serikali inahamisha kutoka bajeti ya mwaka mmoja kwenda mwaka mwingine, kwa mfano hapa tulitegemea Tanga Jiji wawepo, na mashirika mbalimbali,” amesema Maneno na kuongeza:

“Wito wangu kwa viongozi wa netiboli Tanzania wayatengeneze mashindano haya katika kipindi ambacho serikali inatumia fedha zake.

Naye Katibu Mkuu wa CHANETA Judith Ilunda amesema kuwa katika mashindano ya mwaka huu walitegemea zishiriki timu 21 za wanawake na 5 za wanaume lakini sasa hivi timu za wanawake zinazoshiriki ni 12 na nne za wavulana.

Amesema michuano hii iliyoanza tarehe 19 julai itamalizika tarehe 30 juni ambapo Bingwa atapatikana huku washindi wa nafasi za juu wataiwakilisha nchi katika mashindano ya netiboli kwa nchi za Afrika mashariki, huku timu sita za juu zitashiriki kwenye ligi ya netiboli ya muungano ambayo imepangwa kufanyika mjini Zanzibar baadaye mwaka huu.

Katika michezo mingine iliyochezwa jana, Timu ya Magereza ya Morogoro iliifunga kwa tabu Uhamiaji ya Dar es salaam magoli 37-36, huku Mbeni JKT ikiifunga Polisi Arusha magoli 66 Polisi Arusha 63.

Mashindano haya yataendelea tena hapo kesho kwa michezo kadhaa ikiwemo mchezo kati ya timu ngumu ya TAMISEMI QUEENS dhidi ya Polisi Arusha.

No comments:

Post a Comment