Tuesday, 13 July 2021

WAZIRI UMMY AWATAKA MAKATIBU TAWALA WASAIDIZI KUTIMIZA MAJUKUMU YAO

 


Na. Angela Msimbira KATAVI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)  Mhe Ummy Mwalimu(Mb) amewaagiza Makatibu Tawala wasaidizi wa  Mikoa  yote nchini kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kikamilifu kwa weledi kwa kuzishauri, kuzisimamia  na kutoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa bila uoga ili waweze kutimiza majukumu yao kikamilifu.


Ametoa maagizo hayo leo katika kikao na  Sekretarieti ya Mkoa wa Katavi kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya maendeleo katika maeneo ya afya ya msingi, elimu ya msingi na sekondari na  miundombinu ya barabara pamoja na ukusanyaji wa mapato  na matumizi katika Halmashauri katika Mkoa wa Katavi.


Waziri Ummy amesema  Makatibu Tawala wasaidizi wa Mikoa ni wakubwa  zaidi kuliko Wakurugenzi wa Halmashauri, hivyo  wanawajibu wa kuhakikisha wanawasimamia  na kuwapa maelekezo ili kuweza kutoa matokeo chanya katika utekelezaji wa majuku yao ya kutoa huduma bora kwa wananchi.


Ameendelea kusema kuwa Makatibu Tawala Wasaidizi  wa Mikoa wanawajibu kuzisimamia, kuzishauri na kutoa maelekezo  kwa  Halmashauri 184  ili Ofisi ya Rais-TAMISMI  kuendelea kutafuta rasilimali watu, rasilimali fedha na kupanga mikakati ya maendeleo itakayotekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.


Waziri Ummy amesema kuwa Wataalam wa Mikoa ndiyo injini  ya kusimamia utekelezaji wa Miradi ya maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo wanawajibu wa kushauri na kutoa maelekezo  ili kuleta maendeleo katika Halmashauri.


“Ninawaagiza kuhakikisha mnahoji kwa undani bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuangalia vipaombele vya Serikali ambavyo vinasaidia kutatua changamoto za wananchi lengo likiwa ni kuziwezesha hizi Halmashauri kuweza kutimiza majukumu yao” amesema Waziri Ummy


Aidha, Waziri Ummy  amesema katika kuhakikisha  Sekretarieti za Mikoa , Serikali imeteua Wakuu wa Idara  za Mipango  na Uratibu  watano (5) waliofanya vizuri katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuwapeleka Sekretarieti za Mikoa  ili kuhakikisha  kunakuwa na watumishi wenye weledi  na kuondoa dhana kuwa watumishi walioshindikana Wizarani ndio hupelekwa Mikoani.

No comments:

Post a Comment