Na Mwandishi Wetu, Morogoro.


TAASISI ya Elimu Tanzania (TET), imewataka wawezeshaji wa Ujaribishaji wa Mwongozo wa kufundisha Elimu  stadi za maisha za afya  ya uzazi, VVU/UkimwI na jinsia kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kuwa na uzalendo katika kuifanya kazi yao.


Mkurugenzi Mkuu wa  TET, Dkt. Aneth Komba amebainisha hayo leo wakati wa ufungaji wa  mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani hapa kwa siku sita, Ambapo amewaambia washiriki kuwa, mafunzo waliyoyapata  yawe chachu  katika utaoji wa Elimu ya Afya ukiwemo maambukizi ya VVU/UKIMWI, ukatili  na unyanyasaji wa kijinsia nchini.


"Ningependa ifahamike kwa sasa Miongozo hii ipo kwenye majaribio. Wawezeshaji wakati mnapofanya ujaribishaji mnapaswa kufuatilia na kupata mrejesho ya kipi kinahitajika katika kufanyiwa marekebisho". Alisema Dkt. Aneth Komba.


Dkt. Aneth Komba ameongeza kuwa, TET kwa kushirikiana na  Shirika la UNESCO,TACAIDS, Maria Stops na shirika la Room to Read watafuatilia kwa karibu ujaribishaji wa miongozo hiyo katika Halmashauri zote 13 zilizopangwa kufikiwa.


Naye mwakilishi kutoka Wizara ya OR-TAMISEMI, Bi.Teresia amesema kuwa  miongozo hiyo itasaidia katika kupunguza ama kumaliza kabisa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa wahusika watakaopatiwa Elimu hiyo ya stadi za maisha.  


"Tunaamini mafunzo yatasaidia wanafunzi kuweza kupambana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo wanafunzi wengi kushindwa kumaliza shule.


TAMISEMI imefurahishwa na kuona walimu wengi wameweza kupata mafunzo hayo ambayo kwa vitendo na kuwa kila Shule itaweza kuwa na walimu wawili wawilii kwa Shule za Msingi na Sekondari na wataweza kufundisha stadi za maisha kwa wanafunzi." Alisema Bi. Teresia. 


TET iliandaa mafunzo hayo maalum ya siku sita na kuwashirikisha jumla ya washiriki 46 wakiwemo Walimu, Maafisa kutoka TAMISEMI, Wakufunzi na Wataalamu wa afya ambapo lengo ni kuwawezesha jumla ya walimu 1696 wa shule za Msingi na Sekondari kwenye mafunzo katika Halmashauri 13 nchini.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: