Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uboreshaji Maadili kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi Tanzania (WoLaOTa) , Samwel Olesaitabau, akizungumza na waandishi wa habari juzi.


Na Dotto Mwaibale, Singida


TAASISI ya Uboreshaji Maadili kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi Tanzania (WoLaOTa) yenye makao yake makuu mkoani hapa imemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta ya elimu kwa kuwa  na makundi mawili ya wakaguzi wa elimu. 

Ombi hilo limetolewa na  Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Samwel Olesaitabau katika mkutano wake na waandishi wa habari mkoani hapa juzi wakati akitoa maoni yake kuhusu siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwa madarakani.

"Kwa niaba ya Bodi ya WoLaOTa nampongeza Rais Samia katika kuunda Serikali yake yupo makini na ameanza vizuri na mara nyingi nyota njema ni ya asubuhi," alisema Olesaitabau.

Olesaitabau alisema wanamuomba Rais Samia kuboresha sekta hiyo kwa kuweka wakaguzi au wadhibiti ubora wa elimu wenye sifa na wawe katika makundi mawili la  wale watakao kuwa wakifanyakazi hiyo kwa shule za sekondari na kwa shule za msingi katika wilaya na kuwaondoa wale wa kanda na wapewe nguvu ya kisheria kuwashughulikia  moja kwa moja wale wanaopewa taarifa ya ukaguzi kwenye halmashari ambao ni Mkurugenzi na Afisa Elimu.

Alisema zamani wakaguzi hao walikuwa wakichaguliwa kwa kigezo cha mwalimu kuwa kazini sio chini ya miaka 10 na matokeo mazuri ya masomo waliokuwa wakifundisha tofauti na sasa ambapo wanachukuliwa kujiunga na idara hiyo muhimu moja kwa kutoka chuo kikuu pasipokuwa na uzoefu wowote.

"Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000 ndipo wataalamu hawa wamekuwa wakichukuliwa bila ya kuzingatia vigezo stahili jambo ambalo linachangia kufifisha ubora wa elimu," alisema Olesaitabau.

Akizungumzia suala la biashara na utendaji wa kazi kwa watumishi wa umma alisema Rais Samia ameleta matumaini mapya kwa wafanyabiashara wa juu, kati na na wachini na kuwa amerudisha nyuso zilizokuwa zimepondeka kwa wafanyakazi  na sasa nyuso zao zimenyooka na kuwa na matumaini makubwa kwake. 

Olesaitabau alisema kuna watumishi wa umma  wilayani wamekalia viti kwa zaidi ya miaka 15 bila ya kutoa matokeo ni vyema ufanyike utaratibu wa kubaini matokeo ya kazi walizofanya kwani huko kwenye wilaya ndiko Serikali ilipo hivyo wanamuomba achukuwe hatua.

Olesaitabau alitumia nafasi hiyo kuwaomba watanzania kwa imani za dini zao wamuombee Rais Samia kwa Mungu ili atufikishe pale pazuri alipopanga huku akiwaomba wateule wake wote wafanye kazi kwa uadilifu na kila mmoja wao alenge kuwakomboa watanzania kuondokana na ujinga, maradhi na hata umaskini.

Share To:

Post A Comment: