NA.SALEH RAMADHANI.


Vijana washauriwa kutumia mitandao ya kijamii vizuri kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla


Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Kenani Kihongosi amewataka vijana kutumia mitandao ya kijami vizuri na siyo kuitumia vibaya.


Hayo yamebainishwa leo Juni 25,2021 jijini Dodoma wakati akizungumza na vijana wa umoja huo kwenye hafla fupi ya kukaribishwa kwake Makao Makuu mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo hivi karibuni.


Kihongosi amesema, vijana wengi hapa nchini wamekuwa wakijihusisha vibaya na mitandao ya kijamii kwa viongozi,kudhalilishana, kudhihaki jambo ambalo ni kinyume na ukiukwaji wa sheria za chama cha mapinduzi na Taifa kwa ujumla.


"Katika mitandao kuna mijadala isiyo na tija kila mmoja atumie mitandao vizuri,Badala ya kushinda kwenye mitandao bila tija niwasihi kutumia mitandao hiyo kutangaza miradi ya Serikali inayotekelezwa kwenye eneo unaloishi huku ukitafuta fursa za ajira jambo ambalo litawafanya kuchochea maendeleo kwa jamii,"amesema Kihongosi.


Aidha, ameutaka umoja huo kuepuka migogoro katika kazi hususani majungu,dharau na ugomvi ambayo yamekuwa kero kubwa bali wadumishe umoja , upendo na mshikamano viwe nguzo ili kulitumikia Taifa.


Katika hatua nyingine amekemea kwa vikali baadhi ya vijana ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwabeba na kuanza kuwanadi wagombea kabla ya muda wake jambo ambalo sio sahihi na utaratibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kudai wasubiri mwakani ili waanze kampeni.


Vilevile amewataka viongozi wa umoja huo kutembelea sehemu zenye changamoto za vijana kama wafanyakazi wa hotelini,madereva bajaji,bodaboda, na mama ntilie ,machinga ,mafundi ujenzi, umeme, wakulima, wavuvi, pamoja na makundi yote ili kujua changamoto wanazokumbana nazo na kuzifikisha kwenye chama ili zipatiwe ufumbuzi kwa maslahi ya Serikali.


"Niwatake viongozi huko mikoani na wilaya zote kufika kwenye halmashauri za wilaya muongee na wakurugenzi namna ya kupewa zile asilimia zinazotengwa kuwakopesha vijana bila riba ili waweze kufanya biashara mbalimbali na kujikwamua kiuchumi kwani fedha hizo zimekuwa zikitumika kwa watu wengine,"amesema Kihongosi.


Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye Ulemavu ,Ummy Nderiananga amewataka vijana kuchangamkia fursa zinazowazunguka na kuacha mara moja mazoea ya kuishi Bila kuwa na Dira ya Maisha yao.


Mwisho. Up

Share To:

msumbanews

Post A Comment: