Angela Msimbira, SHINYANGA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu ameagiza kusimamishwa kazi wakuu wa Idara Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kwa  kushindwa kusimamia kwa weledi ukamilishaji wa  ujenzi wa Machinjio  ya kisasa iliyopo Ndembezi mjini Shinyanga ili kupisha  uchunguzi kwa tuhuma zinazowakabili.


Akikagua mradi huo leo katika ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga Waziri Ummy amesema kuwa amewasimamisha kazi wakuu hao wa idara kwa kushindwa kutimiza wajibu wao wa kumshauri Mkurugenzi kuhusu mradi huo na kushindwa kusimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.


Amewataja waliosimamishwa kupisha uchunguzi kuwa ni aliyekuwa Kaimu Afisa Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji Bw. Gwakisa Mwaisyeba, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Dkt Tito Kagize, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi Kassim Thadeo na Mkuu wa Kitengo cha manunuzi  Bw.Godfrey Mwangailo na amemuagiza Mkuu wa Mkoa Bw.Dkt Philemon Sengati kuhakikisha anaunda tume itakayochunguza  ubadhilifu wa fedha ambao umesababisha kusuasua kwa ujenzi wa Machinjio hiyo.


Waziri Ummy  amesema kutokamilika kwa  Mradi wa Machinjio ni aibu kwa watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya  Shinyanga  na inarudisha nyuma maendeleo ya Manispaa hiyo.


‘Ukamilishaji wa machinjio hii kutasaidia  kuongeza mapato ya  wananchi na Halmashauri kwa ujumla kwa kuwa Halmashauri ikikusanya mapato  itaweza kutatua changamoto  katika Sekta ya Afya, Elimu na miundombinu ya barabara’ alisema


Mbali na kuwasimamisha Wakuu hao wa Idara  pia ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga  kuwaandikia barua  Mkandarasi wa mradi huo , Kampuni ya Home Africa pamoja na Mhandisi  mshauri  B.J Amour nao wapelekwe  bodi ya Mkandarasi  ili iwawajibishe.


“ Mradi huu haukusimamiwa vizuri na tunawatesa  watu wa shinyanga  mpaka leo  haujakamilika  na fedha hazionekani, kuna shilingi milioni 800 zimelipwa  kwa wakandarasi bila kuhakikiwa  wala kujiridhisha. Huu mradi ni aibu kwa Shinyanga kwa hiyo nawasimamisha kazi kwa wiki mbili  ili wapishe uchunguzi” amesema Waziri Ummy


Katika hatua nyingine Waziri Ummy amesema kuwa  mradi huo  ulitengewa kiasi cha shilingi  bilioni 5.7 lakini hadi sasa  zimetumika  kiasi cha shilingi  bilioni  5.1 na shilingi milioni 600 hazijulikani  zilipo wakati mradi haujakamilika, amesisitiza  kuwa katika ripoti ya mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG)  ilieleza kuna ufisadi na mradi haukukamilika vizuri.  


Hatua hiyo ya Waziri Ummy imekuja baada ya Mstahiki  Meya wa Manispaa ya Shinyanga  Mhe. David Nkulila  kueleza kuwa  kamati ya fedha ya halmashauri hiyo kupitia baraza la madiwani walikuwa wameanza kuchukua hatua baada ya kubaini kuwa thamani  ya fedha katika mradi huo hairidhishi, huku akibainisha  kuwa kupitia vyanzo vya ndani  watatenga shilingi milioni 172 kwa ajili ya kukamilisha machinjio hiyo.


Machinjio hiyo ilianza kujengwa mwaka 2018 na ilitazamiwa kukamilika  mwaka2019  na kuanza kutoa huduma  lakini maendeleo yake yamekuwa  yakisuasua  na kusababisha baadhi ya viongozi kuilalamikia.

Share To:

Post A Comment: