Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI 


OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imepata kibali cha ajira za walimu wa shule ya msingi na sekondari 6,949 na kada mbalimbali za afya 2,726 watakaoajiriwa chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.


Maombi ya ajira hizo yataombwa kwa njia ya mtandao kuanzia Mei 9 hadi 23, mwaka huu kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ummy Mwalimu, amesema ajira hizo zitajaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokoma utumishi kutokana na sababu mbalimbali.


“Serikali imetoa kibali, maana mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza kwamba atatoa ajira 6000 kwa walimu tulikuwa tunapata msukumo mkubwa kutoka kwa wananchi wakihoji kwanini TAMISEMI hatutangazi, taratibu za serikali lazima tupate kibali Menejimenti ya Utumishi wa umma,”amesema.


Hata hivyo, amesema serikali imetoa fursa kwa waombaji ambao ni walemavu kutuma maombi yao kwa nakala ngumu na yaeleze aina ya ulemavu wao na picha zao na kutumwa kwa anuani ya Katibu Mkuu TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu ili aione Mkurugenzi wa kitengo cha watu wenye ulemavu.


Akitaja sifa za waombaji wa ualimu, Waziri Ummy amesema kwa shule ya msingi wanatakiwa walimu wenye daraja la IIIA kuwa astashahada ya elimu ya msingi, elimu ya michezo, elimu ya awali na elimu maalum.


“Mwalimu wa daraja la IIIB anatakiwa kuwa mhitimu wa stashahada ya ualimu wa elimu ya awali, msingi, elimu maalum na Mwalimu wa daraja la IIIC, mhitimu wa shahada ya ualimu masomo ya lugha ya kiingereza, historia na jiografia,”amesema.


Kadhalika, amesema kwa shule za sekondari wapo kwenye makundi manne ambapo anatakiwa mwalimu wa daraja IIIB ambaye amehitimu stashahada ya ualimu wa masomo ya Fizikia, Hesabu, Baiolojia na Kemia.


“Pia mwalimu wa daraja IIIC ambaye amehitimu ualimu aliyesomea elimu maalum kwa masomo hayo na shahada ya ualimu wa masomo hayo, pia awe amehitimu stashahada ya uzamili katika elimu lazima awe mwenye shahada ya kwanza yenye masomo tajwa,”amesema.


Pia amesema kwa waombaji wa ajira hizo ambao wamesomea elimu ya sekondari nje ya nchi wanatakiwa kupata namba ya ulinganifu wa matokeo inayoanzia na herufi EQ…kutoka Baraza la Mitihani la Tanznaia ili kuingia kwenye mfumo wa maombi ya ajira.


“Pia wanatakiwa kupata ithibati ya masomo yao kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ili vyeti vyao vitambulike na kupata uhalali wa kutumika nchini,”amesema.


Pamoja na hayo, Ummy amesema kada za afya ambazo serikali itaajiri ni daktari daraja la II, daktari wa meno daraja la II, tabibu daraja la II, tabibu msaidizi, tabibu wa meno daraja la II, tabibu meno msaidizi, mfamasia daraja la II.


Nyingine ni mteknolojia wa dawa daraja la II, mteknolojia msaidizi wa dawa, mteknolojia wa maabara daraja II, mteknolojia msaidizi maabara, mteknolojia mionzi daraja la II, mteknolojia msaidizi wa mionzi, mteknolojia wa macho daraja la II.


Kadhalika, alisema itaajiri Ofisa Muuguzi daraja la II, Ofisa muuguzi msaidizi daraja la II, Muuguzi daraja la II, mtoa tiba kwa vitendo daraja la II, Ofisa afya mazingira daraja la II, Ofisa afya mazingira msaidizi daraja la II, Msaidizi wa afya, Katibu wa afya daraja la II, Ofisa ustawi wa jamii daraja la II na Ofisa lishe daraja la II.


Amesema ajira zitatolewa kwa haki na hataruhusu kuwepo na aina yeyote ya ushawishi  na kusisitiza watazingatia wale waliomba kwa maelekezo yaliyotolewa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: