MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM) kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema Lugangira akiwa Bungeni Jijini Dodoma leo

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Profesa Kitila  akijibu hoja mbalimbali

NA MWANDISHI WETU, DODOMA.

MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM) kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema Lugangira ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara itoe Kanuni za Food Labelling zitakazowalinda walaji na sio kuendelea kuweka maisha ya Watanzania rehani.

Ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Mchango wa Maandishi na Taarifa aliyotoa ambapo alisema hilo linatokana na hivi sasa kuwepo kwa changamoto ya Usalama wa Chakula yaani Food Safety unaochangiwa na baadhi ya majukumu ya TFDA ya kupelekwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Akichangia kupitia Mchango wake wa Maandishi Mbunge Neema Lugangira alianza kwa kuikumbusha Wizara ya Viwanda na Biashara kuwa moja ya majukumu yake ni kufuatilia na kutathimini utendaji katika viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo vidogo na biashara ndogo ndogo ikiwemo taasisi zinazowezesha maendeleo viwanda na biashara.

Alisema sanjari na jukumu hilo baada ya Marekebisho ya Sheria ya Viwango ya Mwaka 2009 iliyochukua majukumu ya TFDA na kuyahamishia TBS ikiwemo jukumu la kusimamia Ubora na Usalama wa Chakula .

Aidha alisema Wizara ya Viwanda na Biashara  imefanya kazi kubwa ya kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata na kusindika vyakula nchini na inastahili pongezi kubwa lakini kuna changamoto katika eneo la Usalama wa Vyakula nchini.

“Nasema hivi kwa sababu nyanya inaweza kupuliziwa dawa siku kama ya jana na ikavunwa leo leo au kesho nyanya hiyo ikiuzwa sokoni mwananchi akainunua na kutengeneza kachumbari na akala jambo ambalo linaweka hatarini maisha yake kutokana na chemikali hatari zilizopo kwenye nyanya” Alisema

Mbunge Neema Lugangira aliongeza kuwa wakati mwengine wananunua juisi ya box kama ya juisi ya chungwa wakiamini juisi ile ni ya chungwa halisi lakini mara nyingi kinachokuwepo ndani ni Concentrate, rangi, ladha na sio chungwa halisi pia kiwango cha sukari kinachokuwepo ni hatari sana.

“Huu ni mfano ambao unaweza kupelekea udanganyifu mkubwa unaochangia kwa kasi ongezeko la tatizo la uzito uliozidi na viribatumbo nchini hususan kwa watoto wadogo ambao ni wanywaji wakubwa wa juisi ni za box.

Katika mfano mwingine Mbunge Lugangura alisema wananchi tunanunua Yoghut ya Strawberry tukiamini ndani kuna Strawberry halisi jambo ambalo mara nyingi sio kweli bali kinachokuwepo ni rangi na ladha japo kwenye kopo la Yoghurt/Mtindi inakuwepo picha ya tunda la Stawberry.” Alisema

Mbunge alisema hali hiyo ipo hata kwenye bidhaa za vyakula zingine ikiwemo mafuta ya kupikia, ice cream ambapo changamoto hiyo inawezeshwa kwa kiasi kubwa na Mfumo wa sasa wa kuweka lable/lebo kwenye Vifungashio vya Chakula yaani Food Labelling; jambo ambalo linaweza kuhatarisha Maisha ya Watanzania kwa sababu hivi sasa wengi wetu tunanua bidhaa za vyakula pasipo kuelewa nini haswa kimo ndani yake hivyo hatujui usalama wake.

Aliongeza kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara inalo jukumu la moja kwa moja la kuimarisha Usalama wa Vyakula vinavyochakatwa na kusindikwa na viwanda na biashara zilizochini ya Wizara na kutokufanya kitu na kuendelea kuweka Maisha ya Watanzania Rehani.

"Kwa mantiki hiyo ningependa kukushauri wewe kama Waziri wa Viwanda na Biashara uandae Kanuni za Food Labelling zitakazoweka ulazima wa wachakataji na wasindikaji wa vyakula kuandika wazi kilichopo ndani na takwa hilo liwe kwa bidhaa za vyakula zinazozalishwa nchini na zinazotoka nje ya nchi” Alisema Mbunge Lugangira 

Hata hivyo alisema kama wameweza kufanya hivyo kwa Sigara ambazo juu yake pakiti inasema wazi uvutaji wa sigara ni hatari kwa maisha yako kwanini wasindwe kwenye bidhaa za vyakula?

Mbunge Neema alisisitiza pia umuhimu wa Wizara kuanzisha Kampeni ya Elimu kwa Umma ya kuwaelimisha jamii maana ya Food Labelling watakazopendekeza kupitia Kanuni ili kila Mtanzania aweze kufanya maamuzi sahihi kutokana na manunuzi ya chakula jambo ambalo hata Chama cha Mapinduzi imegusia kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2020-2025 Ibara ya 49(7) ukurasa wa 61 kwa kusema "CCM itaelekeza Serikali kubuni na kuendeleza mikakati ya uhamasishaji wa Watanzania kupenda kutumia bidhaa zinazozakishwa katika viwanda vya ndani" na hii lazima iende sanjari na kumlinda mlaji atakae nunua bidhaa za vyakula. 

Mbunge Neema Lugangira alimalizia kwa kusema ni matarajio yake Wizara ya Viwanda na Biashara itafanyia kazi ushauri wake na Tanzania inaweza kujifunza toke nchi zingine kama Chile.

Wakati wa kuhitimisha Hoja yake ya Bajeti, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Profesa Kitila Mkumbo aligusia Ushauri aliotoa Mbunge Lugangira wa kuandaa Kanuni za #FoodLabelling na kuahidi kuliangalia na kuondoa mapungufu yaliyopo.


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: