Na,Jusline Marco;Arusha


Wadau wa utalii Mkoani Arusha wameiomba mamlaka ya hifadhi Ngorongoro kutatua changamoto za kimiundombinu zilizopo ndani ya hifadhi hiyo pomoja na kuweka mipango madhubuti katika uendeshaji wa website ili kuweza kuboresha sekta ya utalii nchini.


Wakizungumza katika kikao cha wadau wa utalii na mamlaka ya hifadhi Ngorongoro,wadau hao wamesema kuwa ubovu wa barabara zilizopo ndani ya hifadhi hiyo ni changamoto kwa watalii ambapo kwa pamoja wameiomba mamlaka hiyo kufanya marekebisho ili kuwezesha magari kupita kwa urahisi hasa nyakati za mvua.


Aidha wadau hao wameiomba mamlaka hiyo kupitia mfumo wa vyama vyao kuona ni kwa namna gani wataweza kuwashika mkono kwa kuwapatia mkopo wa riba nafuu au usiokuwa na riba kabisa na hii ni kutokana na tatizo la Covid lililowapelekea wadau hao kukosa ajira kwa muda mrefu.


"Endapo Mamlaka itatusaidia mkopo kama wadau tutaweza kuzihudumia familia zetu kwa kipindi hiki ambapo ugonjwa wa Covid umekuwa chanzo cha watalii kupungua  nchini na kusababisha baadhi ya wadau wa utalii kukosa fedha za kuendesha kampuni zao na kuhudumia familia zao kwa kukosa kipato."Alisema mdau huyo 


Kwa upande wake Kamishna Msaidizi huduma za Shirika,Audax Rwezaura Bahweitima alisema kuwa ipo kamati ambayo itaundwa kwaajili ya kushughulikia changamoto mbalimbali katika sekta ya utalii ikiwemo ugonjwa wa  COVID 19 katika sekta ya utalii ili kuwawezesha wadau wa utalii kuweza kirudi katika mpangilio wa awali.


"Sisi kazi yetu tuliyonayo kubwa ni kama mamlaka ya serikali ni kuyachukuwa yale ambayo yanaonekana ni kikwazo na kuyapandisha kwenye ngazi husika na kufikishwa pale ambapo panastahili".Alisema Kamishna Rwezaura


Sambamba na hayo Meneja wa Utalii wa Mamlaka hiyo Paul Hilonga Fisoo aliwataka wadau hao kutumia maeneo rasmi katika utoaji wa zawadi kwa wakazi walio ndani ya  hifadhi hiyo hisusani watoto pindi wanapokuwa na wageni ili kuepuka uharibifu wa mali unaoweza kutokea kwa watalii wengine ambao hawatakuwa na zawadi za kuwapa.


Hata hivyo lengo la kikao hicho ni kukumbushana majukumu baina ya wadau wa utalii pamoja na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro,kujenga mahusiano yaliyo bora pamoja na kurekebisha mambo mbalimbali yakiwemo ya kimfumo,kisera na taratibu zilizopo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: