Thursday, 18 February 2021

Wananchi Wa Vijiji 6 Katika Hifadhi Ya Ngorongoro Wanufaika Na Mradi Wa Simba.

Wananchi kutoka vijiji vya kata ya Ngorongoro wakiwasilikilza wataalam wa utafiti wa Simba kutoka shirika la Kopelion Inc kuhusu faidaa za uhifadhi wa Simba kabla ya kupewa malipo ya motisha katika mradi wa uhifadhi wa Simba.


Mratibu wa Mradi wa Simba kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Bashir Nchira akizungumza na wananchi wa kata ya Ngorogoro na Misigyo kabla hawajakabidhiwa malipo ya Motisha kwa ajili ya uhifadhi wa Simba.



Muanzilishi na mtafiti mkuu wa Shirika la Kopelion Inc Bibi Ingela Janssan maarufu kama ‘mama Simba’ akiongea na wananchi wa kata ya Ngorongoro kuhusu mradi wa kuhifadhi Simba katika maeneo yao wakati wa Sherehe wa kukabidhi hundi kwa wananchi wa vijiji vitatu vya kata hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Kopelion Inc Dkt. Bernard Kissui (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mokilal Bw. Osoi Nitwati (kulia) ikiwa ni malipo ya motisha kwa ajili ya Uhifadhi wa Simba.

 Na Kassim Nyaki-NCAA


Wananchi kwa vijiji sita katika kata za Ngorongoro na Misigyo wanaoshi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamenufaika na mradi wa simba kwa kupata shilingi milioni 3 kwa kila Kijiji kutoka shirika la Kopelion Inc.

Kwa mujibu wa muanzilishi na mtafiti mkuu wa Shirika la Kopelion Bibi Ingela Janssan maarufu kama ‘mama Simba’ vijiji viliovyonufaka na mradi huo ni Olorobi, Kayapus na Mokilal kutoka kata ya Ngorongoro na Vijiji vya Misigyo, Loongoijoo na Kaitakiteng kutoka kata ya Misigyo.

Kwa mujibu wa Ingela Janssan mradi huo ulianzishwa mwezi oktoba mwaka jana kama sehemu ya majaribio kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa ajili ya Uhifadhi wa Mnyama Simba kupitia ushirikishwaji wa Jamii kwa lengo la kupunguza mgogoro wa wananchi na Simba katika maeneo ya hifadhi.

“Miaka 100 iliyopita duniani kote ilikadiriwa kuwa na simba 200,000, lakini kwa sasa inakadiriwa kuwa na Simba 20,000 utaona kwa kiasi kikubwa simba wamepungua kwa miaka 25 iliyopita, hivyo Shirika letu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wadau wengine tunashirikiana na jamii zilizoko maeneo ya Hifadhi kumlinda simba na kutomuona kama adui wa mifugo na maisha ya watu ili Simba wazidi kuongezeka” amesema Ingela.

Ingela ameongeza kuwa kupitia uhifadhi shirikishi Shirika lake kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali linatoa malipo ya motisha kwa ajili ya Uhifadhi wa Simba ambapo wananchi wanapomuona katika maeneo ya makazi yao wanapaswa kutoa taarifa ya uwepo wa Simba hao bila kuwadhuru na utaratibu huo unalenga kupunguza migogoro ya Wananchi na mnyama simba (human-Lion Conflict).

Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi Shirika la Kopelion Dkt. Bernard Kissui ameleza kuwa kihistoria Simba walikuwa wengi sana duniani lakini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali idadi yao porini imekuwa ikipungua kutokana na mgogoro ya Simba na binadamu hasa Simba wanapokula mifugo ya Wananchi na kuongeza kuwa shirika la Kopelion lina lengo la kujenga mahusiano ya kijamii kupitia program ya Uhifadhi Shirikishi.

“Mdadi huu ulianza mwaka jana na tuliamua kuanza na kata mbili kama sehemu ya majaribio kwa miaka mitatu ijayo, miezi minne iliyopita tumeona imeleta manufaa makubwa kwa jamii kuhamasika katika mradi huu ndio maana leo tumetoa malipo ya motisha kwenye vijiji sita vya kata 2 na kadri mradi utakavyofanikiwa tutaongeza maeneo mengine” aliongeza Dkt Kissui.

Dkt Kissui amefafanua kuwa utoaji wa malipo kwa wananchi wa kata hizo mbili ni faida inayotokana na kuwepo na Simba katika jamii ambapo utaratibu huo unalenga kungeza idadi ya Simba kupitia uhifadhi Shirikishi ili Simba waendelee kuwepo na Jamii izidi kunufaika badala ya kumuona Simba kama adui yao.

Mratibu wa Mradi huo kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw, Bashir Nchira ametoa rai kwa wanufaika wa Mradi huo kuutekeleza kwa ufanisi na uzalaendo ili waendelee kupata faida za mradi kupitia Hifadhi ya Ngorongoro na wadau wa maendeleo.

“Kupitia ushirikishwaji huo huko tuendako Simba atazidi kuonekana rafiki wa uhifadhi na si uadui, Nawaomba muendelee kutoa ushirikiano kwa mashirika mbalimbali yanayofanya tafiti za wanyamapori ndani ya hifadhi yetu” alisema Nchira.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ameupongeza mradi huo na kushauri shirika hilo kuongeza mradi wa Wanyama wengine kama Fisi na Tembo ambao pia wamekuwa wakichangia migogoro na wananchi. Aidha amewaasa viongozi wa vijiji vilivyonufaika na mradi huo kuhakikisha wanabuni miradi yenye tija itakayosaidia wananchi na kuhakikisha hakuna ubadhirifu ktika mradi huo


No comments:

Post a Comment