Serikali imesema kamwe haitakuwa kikwazo kwa wawekezaji katika kutoa vibali vya Tathmini ya Athari kwa mazingira katika kuwezesha uwekezaji na maendeleo ya viwanda.

Kauli hii imetolewa hii leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano ana Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa lengo la kukagua shughuli za utunzaji na Uhifadhi wa Mazingira

Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa inaweka mazingira Rafiki kwa wawekezaji na kutoa miongozi katika hifadhi ya mazingira na kuliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutoa ushauri wa kitaalamu kuwezesha wawekezaji kuzingatia Sheria.

“NEMC simamieni Sheria ya Mazingira, Viwanda visiwe sehemu ya uchafuzi wa Mazingira ili Maendeleo ya Viwanda yaendane na Hifadhi ya Mazingira pia NEMC msifanye kazi ya upolisi kwa kufunga Viwanda na kutoza faini kubwa, kaeni na wenye Viwanda waelekezeni kuzingatia Sheria” Waziri Ummy alisisitiza.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemuagiza Mkurugenzi wa Mji Kibaha kuhakikisha katika Mipango na Bajeti wanatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa dampo la kisasa pamoja na kutoa elimu kwa wananchi namna bora ya kutenganisha taka kuanzia ngazi ya kaya.

“Mkurugenzi, taka ni mali, si kila taka ziende dampo, wekeni utaratibu kwenye vizimba kwa kutenganisha taka za plastiki, taka za majumbani na taka zinazoweza kurejerezeka ili wenye viwanda vya plastiki na vile vya kutengeneza mbolea waweze kupata malighafi” Ummy alisisitiza.

Akimkaribisha katika Mkoa wa Pwani Mkuu wa Mkoa Mhandisi  Evarist Ndikilo amesema Mkoa wake unakabiliwa na changamoto kubwa ya ukataji miti kutokana na matumizi ya kuni na mkaa na kutoa rai kwa Wizara kuangalia uwezekano wa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ikiwemo gesi.

Pia ameshauri kuwekwa kwa utaratibu kwa wachimbaji wa mchanga kuhakikisha kunakuwa na urejerezaji wa maeneo ya machimbo kwa kupanda miti ili kuepuka uharibifu wa Mazingira.

Waziri Ummy amesisitiza kuwa Agenda ya Mazingira ni suala mtambuka na kutoa rai kwa uongozi wa Mkoa wa Pwani kutumia Sheria ndogo za Halmashauri kusimamia suala la upandaji miti kwa kuanzisha vitalu vya miche.

Katika siku ya kwanza ya Ziara ya Waziri Ummy Mwalimu Mkoa wa Pwani ametembelea Dampo la Mji Kibaha, Kiwanda cha Futan Mining kinachojihusisha na uchenjuaji wa madini ya Kopa na Kiwanda cha Prance International Ltd.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: