NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.


Baadhi ya wananchi wa halmashauri ya Arusha DC wameishukuru serikali kwa kueendelea kuimarisha maisha ya wananchi wenye kipato cha chini kupitia ruzuku ya fedha zinazotolewa  kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini mradi  unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF awamu ya III.


Mmoja wa wananchi hao Leonia Nestori (64) mkazi wa kijiji cha Oloirien kata ya Oloirien akizungumza wakati wa zoezi la kupokea ruzuku hizo alisema kuwa kabla ya kwenye mpango huo wa TASAF maisha yalikuwa magumu sana kwani walishindwa kumudu kupata mahitaji ya muhimu ya familia kama malazi, chakula na mavazi.


 Alisema kuwa fedha wanazozipata mara kwa mara zimewasaidia kumudu kupata mahitaji ya familia pamoja na kupata mahitaji ya shule kwa watoto kwani kupitia fedha hizo wameweza kuanzisha miradi midogo ya kilimo na mifugo tofauti na hapa awali kabla ya neema ya mpango wa TASAF kuwashukia.



Alifafanua yeye binafsi fedha hizo zimemuwezesha kumudu kujikimu kimaisha na wajukuu zake ambao, amelazimika kuishi nao mara baada ya wazazi wao kufariki dunia na kubaki yatima.



"Mimi TASAF imenisaidia sana katika kuendesha maisha ya familia yangu, fedha ninazopokea nanunulia  mahitaji ya  shule ya wajukuu zangu, ambao ni yatima, kabla ya TASAF wajukuu zangu wangeweza hata kuacha shule, nilishindwa hata kuwanunulia nguo, kalamu, daftari na mahitaji mengine ya shule, kwa kweli, tunamshukuru Rais wetu Magufuli, ametuokoa sisi masikini" ameweka wazi Leonia. 



Loisojake Sangeti (74) mkazi wa Olosiva, amesema kuwa, kabla ya mradi huo wa TASAF, maisha yalikuwa magumu sana, lakini sasa TASAF imewezesha kaya nyingi kujikimu kimaisha kwa kutumia fedha hizo kununua kuku, mbuzi, kondoo na kuanza ufugaji, mifugo iliyowafanya kuwa na uhakika wa kupata chakula cha familia, pamoja na kununua mahitaji mengine muhimu kutokana na kuuza mifugo na mazao ya mifugo hiyo kama maziwa na mayai.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule amewataka wanakaya hao walioko kwenye mapango wa kunusuru Kaya masikini na wanaopokea ruzuku hiyo kutumia fedha hizo vizuri kwa kuzingatia lengo lililokusudiwa na serikali la kupambana na umasikini uliokithithiri sambamba na kuhakikisha kaya hizo zinaweza kujikimu kwa kupata mahitaji ya muhimu ya familia zao.



"Serikali inatoa pesa hizo kwa ajili ya ruzuku ya msingi ya kujikimu, ruzuku ya elimu kwa ajili watoto wanaosoma, kuwapatia mahitaji yao ya shule na kuhakikisha wanahudhuria shuleni bila kukosa, pamoja na ruzuku ya afya kwa watoto wa chini ya miaka mitano, kuhakikisha wanawapeleka kliniki na kupata huduma stahiki za afya ili kupunguza vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano". Alisema Mkurugenzi Mtambule.


Naye mratibu wa TASAF wa halamshauri hiyo Grace Makema alisema kuwa jumla ya shilingi milioni 423.1 zinatarajiwa kugawiwa kwa kaya 8,223, kwenye vijiji 45 vilivyo kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini, ikiwa ni ruzuku ya kipindi cha  miezi miwili.


Alieleza awali jumla ya kaya 9,107 zilikuwa kwenye mpango wa kunusu kaya masikini Halmashauri ya Arusha ambapo wanakaya 79  wameondolewa kwa kufariki dunia, kaya 55 kuhama maeneo yao ya awali, kaya 4 kupoteza sifa kwa kuwa viongozi wa seriali na kaya 15 kujitoa kwenye mpango kwa hiari kwa kuwa tayari zimejiweza n km huku kaya 541 kutohudhuria kwenye uhakiki awamu mbili zilizofanyika ambapo hivi sasa zimebaki kaya 8,223 ambazo zimepokea ruzuku awamu hii.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: