Na Mwandishi Wetu, KIBAHA


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendelea ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewajia juu baadhi ya wakurugenzi wa halamashauri kwa kushindwa kuzihudumia idara za ardhi katika halmashauri zao na kuzifanya idara hizo kufanya kazi katika mazingira magumu.


Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, uongozi wa mkoa wa Pwani na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo tarehe 31 Desemba 2020 akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kukagua miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika mkoa wa Pwani, Dkt Mabula alisema kuna baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wamekuwa wakorofi na kuziona idara za ardhi kama siyo sehemu ya idara zao na kuziacha bila kuzihudumia.


Alisema, baada ya kutoka waraka uliohamisha Maafisa Ardhi kurudi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuna baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri waliamua kujivua kuzihudumia idara hizo kwa kisingizio kuwa idara hizo sasa haziko chini yao na zimerejeshwa Wizarani.


Dkt Mabula alisema, waraka uliotolewa na kusambazwa kwa Makatibu Tawala wa Mikoa  ulieleza wazi kuwa wajibu wa Wizara ya Ardhi kwa watumishi wa sekta hiyo utakuwa kwenye  masuala ya sera, ajira na nidhamu lakini usimamizi utaendelea kubaki kwa wakurugenzi wa halmashauri.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, majukumu ya kupanga miji ni ya halmashauri za miji , manispaa na majiji hivyo wakurugenzi wa halmashauri bado wana wajibu wa kuzihudumia idara hizo ili ziweze kupanga miji vizuri pamoja na kutoa huduma zinazohusiana na masuala ya ardhi.


‘’Hawa ni watumishi wenu kama walivyo wale wa idara nyingine za afya, elimu nk hivyo mnapaswa kuwahudumia vizuri ikiwemo kuwapatia vitendea kazi ili waweze kufanya kazi vizuri’’ alisema Dkt Mabula.


Aliwataka Wakurugenzi wa Halmashauri kubadilika na kuanza kuzihudumia idara za ardhi vizuri kwa kuzipangia idara hizo bajeti ya kutosha pamoja vitendea kazi kama magari na vifaa vya kupimia ili ziweze  kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Share To:

Post A Comment: