NA MWANDISHI WETU, ,CHALINZE. 


MBUNGE Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete amefanya ziara maalum ya siku moja katika ofisi za Shirika la Umeme Tanzania -TANESCO-Chalinze kwa lengo la kuona utendaji kazi wao na pia kupata ufumbuzi wa kero za Wananchi juu ya huduma hiyo ya nishati.


Akiwa katika ziara hiyo, Mheshimiwa Mbunge Ridhiwani Kikwete alipata wasaha wa kufanya mazungumzo na Kaimu Meneja TANESCO-Chalinze, Elieza Minja na baadae aliweza kutembelea kuona eneo la mitambo ya kupokea na kusambaza umeme ya kisasa (Sub station) eneo ambalo pia kwa sasa lipo kwenye upanuzu ili kuongeza ufanisi.


Katika mazungumzo hayo, Mhe. Mbunge alitaka kufahamu mpango wa shirika hilo juu ya kufikisha umeme katika maeneo ambayo bado hujafika ilikuondoa kero za muda mrefu kwa wananchi wa ndani ya jimbo hilo.


"Lengo kupata taarifa sahihi juu ya maeneo ya Wananchi wetu wa Chalinze ambao hadi sasa  hawajafikiwa na umeme kwani kilio chao kikubwa tukiwa huko kwenye ziara wananiomba umeme.


Lakini pia ni kutaka kufahamu miradi ya umeme ukiwemo mradi wa Umeme Vijijini- REA na umeme Jazilizi ndani ya Jimbo imefikia hatua gani" alisema Mbunge Ridhiwan Kikwete. 


Kwa upande wake Kaimu Meneja, Minja alimtoa hofu Mbunge juu ya suala la umeme kwa Chalinze kwa kumhakikishia kuwa hadi sasa kuna  uwepo wa umeme wa kutosha.


"Chalinze tuna umeme wa uhakika na wa kutosha kabisa na mwamko wa wananchi kuhitaji huduma ya umeme ni mkubwa tumeendelea kujipanga kufikisha huduma maeneo yote.


"Kwa baadhi ya maeneo bado mkandarasi anaendelea na zoezi la kufikisha umeme huko lakini changamoto mkandarasi huyu amekuwa akisuasua hali ambayo imepelekea baadhi wananchi hao  kulalamikia kutofikiwa na umeme" Alieleza Minja.


Aidha, Minja alieleza kuwa, Mkandarasi wa kampuni ya SINO TECH aliyepewa tenda hiyo amekuwa akichelewesha zoezi hilo na amepewa taarifa za mara kwa mara lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.


"Huyu mkandarasi ndiye anayepeleka umeme baadhi ya Vijiji lakini ufanisi wake umekuwa wa chini hali ambayo ofisi imempatia taarifa juu ya hilo kwani anaonekana kutukwamisha" alisema Minja.


Hata hivyo, Mbunge alieleza kuwa katika ziara zake amekutana na malalamiko ya Wananchi dhidi ya mkandarasi huyo hali ambayo ameshauri TANESCO kumweleza Waziri wa Nishati kumchukulia hatua ikiwemo za kumuondoa na kuweka mwingine ilikuwasaidia wananchi wanyonge.


"Nilienda huko Vijiji vya Kata ya Mkange nilikuta kero za wananchi wakimlalamikia huyu mkandarasi. Kero hii si mara moja na wala sio eneo moja maeneo mengi aliyopewa tenda. 


Nashauri kama itawapendeza ni kumuondoa na kuweka mkandarasi mwingine ili wananchi wetu wapate umeme na wafurahie huduma hii ya umeme ili uwaongezee tija katika uzalishaji mali" alisema Mbunge Ridhiwan Kikwete. 


Aidha, akiwa upande wa mitambo ya kituo cha kusambazia umeme alielezwa kuwa, kwa sasa TANESCO wapo kwenye hatua ya kukipanua kituo hiko ili kiweze pia kupokea umeme wa  Kinyerezi na wa Nyerere ambao utafika hapo na kisha kusambazwa Mkoa wa Dar es Salaam na Dodoma na baadhi ya mikoa.


"Kwa sasa tunafanya upanuzi wa eneo la mitambo yetu ambapo pia hapa Sub station ya Chalinze itakuwa ikipokea umeme wa Kinyerezi na wa Nyerere. Mradi huu utaendelea kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi nchini hasa mikoa ya Mkoa wa Pwani, Dar es Salaam na Dodoma" alieleza Minja.


Mbunge anaendelea na ziara yake hiyo katika maeneo mbalimbali ndani ya jimbo.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: