Na Grace Semfuko, MAELEZO

 Ripoti ya kwanza ya mwaka 2019 ya Mpango wa Afrika wa Kujitathmini Kiutawala bora APRM umebaini Tanzania kufanya vizuri kwenye suala la ulinzi na usalama mambo ambayo yametajwa na ripoti hiyo kuwa yamekuwepo tangu kupata uhuru


wa nchi hiyo.

 Ripoti hiyo imeipongeza Tanzania katika kusimamia misingi ya haki za binadamu, usalama wa nchi, ukuaji wa uchumi, matumizi ya lugha ya Kiswahili pamoja na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa zaidi ya miaka 50 mpaka sasa.

 Akizungumza mara baada ya kuwasilisha mada kwenye mkutano wa kitaifa kuhusu ripoti ya Tanzania ya mwaka 2019, Mwenyekiti wa Bodi ya APRM Tawi la Tanzania Profesa Hasa Mlawa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri katika usimamizi wa utawala bora kati ya nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa mpango huo.

 “Tanzania iliandaa ripoti yake ya kwanza ya APRM na kuiwasilisha katika kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki mpango huo Januari 2013 Addis nchini Ethiopia, mwaka 2014 Serikali iliendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto za utawala bora zilizoainishwa kwenye ripoti kupitia mpango wa muda kati ya Wizara, Idara na Wakala za Serikali, Taasisi hizo zimekuwa zikiandaa taarifa za kila mwaka zikigusia maeneo ya  muungano, ardhi, usawa wa kijinsia na huduma za kijamii” amesema Profesa Mlawa.

 Ameongeza kuwa hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Tanzania imekuwa ikijitathmini na kwamba yapo mambo mengi mazuri ambayo yanafanywa na Serikali katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ikiwepo eneo la usimamizi bora wa uchumi na rasilimali za Taifa.

 Naye mtaalamu wa masuala ya kutathmini utawala bora wa APRM Dkt. Rehema Twalib amesema kumefanyika mambo mengi mpaka kufikia hatua ya utoaji wa ripoti hiyo ikiwepo mapitio ya sera za Tanzania za utawala bora katika kuleta maendeleo na hivyo ripoti hiyo imezingatia mambo yote.

 “Katika eneo la usimamizi wa uchumi tunaangalia mwenendo wa sera zetu, hapa tunaangalia je? Sera zetu zimesababisha uwepo wa mendeleo ya kiuchumi kama ambavyo tunaona? Hapa nyie wote ni mashahidi kwamba nchi imepiga maendeleo makubwa mpaka tumefikia kuwa katika uchumi wa kati” amesema Dkt Twalib.

 Mpango wa Afrika wa kujitathmini kiutawala bora APRM ni ajenda maalum ya demokrasia na utawala bora ya Umoja wa Afrika, ulibiniwa na Waafrika wenyewe mwaka 2003 lengo likiwa ni kufanya tathmini ya za utawala bora katika nchi zao, mpango huu umeanzia kwenye maeneo makuu manne ambayo ni demokrasia na siasa, usimamizi na uchumi, utendaji wa Mashirika ya Biashara na Maendeleo ya Jamii.

Share To:

Post A Comment: