Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim  Mjaliwa (Mb)  ametoa siku 15  kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)  na Suma JKT  kuhakikisha  ujenzi wa Hospitali ya  Uhuru  unakamilika ifikapo disemba  5, 2020.


Akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo leo Jijini Dodoma Mhe. Majaliwa amesema Hospitali ya Uhuru ni moja kati ya miradi ya kimkakati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuimarisha  utoaji huduma  katika Sekta ya afya ambayo inaanzia kuboresha kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa na Hospitali za Magonjwa makubwa.


Anaendelea kufafanua kuwa Serikali  imekuwa mstari wa mbele  kuhakikisha inaboresha huduma za afya  kwa lengo la  kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo imejikita katika kuhakikisha miradi yote ya kimakakati  inakamilika kwa wakati ili ianze kutumika

 

“ Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Wakala wa majengo (TBA),  Suma JKT, hakikisheni ujenzi wa Hospitali hii unakamilika kwa wakati, fanyeni kazi usiku na mchana, jengeni vibanda na kuhamia  kwenye eneo la ujenzi, ongezeni wafanyakazi ili kukamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa” amesisitiza  Mhe. Majaliwa


Mhe. Majaliwa amesema miradi ya Kimakakati inatakiwa ikamilike kwa wakati na Watanzania wanahamu ya kuona miradi inakamilika  na kuanza kutoa huduma hivyo fanyeni kazi kwa weledi ili kuweza kukamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo muhimu kwa jamii


Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema ujenzi wa Hospitali ya Uhuru imekadiriwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 3.995 na kiasi kilichotengwa ni shilingi bilioni 3.410 ambapo zaidi ya  shilingi milioni 995 zilikuwa ni fedha za maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika  na shilingi bilioni 2.415 ni gawio la kampuni ya simu ya Airtel.


Naye Msaidizi wa Mkuu wa JKT Colonel Laurence Angelo Lupenge amesema mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Uhuru umefikia asilimia 92 na kazi zilizofanyika ni kusafisha eneo la mradi,kuchimba na kujenga msingi, kujenga “frame” ya jengo pamoja na kuta, kupiga “plaster” kuta pamoja na” skimming”, kuweka njia za mifumo ya umeme,kupaua na kufunga gypsum board,kuchimba mashimo ya maji taka na kuweka “rough floor” kwa ajili ya kuweka vigae

Share To:

msumbanews

Post A Comment: