Saturday, 21 November 2020

USWIS WARIDHISHWA NA KAZI INAYOFANYWA NA TFCG NA MJUMITA KATIKA KUHIFADHI MISITU NCHINI.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG ) Charles Meshack akifafanua jambo mbele ya Katibu Tawala  Msaidizi  wa Uchumi na Uzalishaji  wa Mkoa wa Iringa, Elia Luvanda na wadau wengine alipokuwa akieleza lengo la mradi na namna utakavyotekelezwa mkoani humo.
 Muwakilishi wa Balozi wa Uswis nchini Tanzania, Peter Selder ambaye ni Mkuu wa Kitengo  cha ajira na kipato akivishwa nguo ya jamii ya kimasai kama zawadi kwa kufadhili mradi huo.
Wajumbe wa kamati ya ushauri ya Mradi, Wanahabari, Viongozi wa kijiji na wana Kijiji wa Kijiji cha Mahenge wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya majadiliano ya utekelezaji wa mradi huo kwenye kijiji hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA). Rahma Njaidi  akizungumza na Wajumbe na kamati ya ushauri ya Mradi na wananchi wa Kijiji cha Mahenge Wilayani Kilolo Mkoani Iringa.
Muwakilishi wa Balozi wa Uswis nchini Tanzania bwana Peter Selder ambaye ni Mkuu wa Kitengo  cha ajira na kipato akizungumza na wana Kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo alipotembelea kuona maendeleo ya kijiji hicho kipya katika awamu ya tatu ya Mradi alipoambatana wajumbe wa ushauri wa mradi.Na Calvin  Gwabara, Morogoro.


UBALOZI wa Uswis nchini  kupitia Shirika lake la Maendeleo (SDC) umeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali na wadau wengine  katika uhifadhi shirikishi wa misitu ili kuitoa Tanzania kwenye nchi zinazoongoza kwa uharibifu wa misitu duniani.

Hayo yalisemwa na Muwakilishi wa Balozi wa Uswis nchini Tanzania, Peter Selder wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi ya ushauri wa Mradi wa Uhifadhi shirikishi wa Misitu ya vijiji katika Kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo mkoani Iringa kuona maendeleo na ushiriki wa wana kijiji katika jitihada hizo ili kilinda misitu na kunufaika na rasilimali zinazotokana na uhifadhi huo.

Selder alisema ameridhishwa mbinu inayotumiwa na  Shirika la Shirika la kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG)  na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA)  ya kuwajengea uwezo jamii, viongozi na wadau wengine jinsi ya kuilinda, kuihifadhi na kisha kunufaika na mazao ya misitu hiyo moja kwa moja kupitia shughuli mbalimbali.

“ Nimefurahi kuona namna jamii inavyoshiriki na kunufaika moja kwa moja na hii itasaidia sana kwani wanapata motisha ya moja kwa moja kwao binafsi na vijiji na hii inawafanya waone umuhimu wa kuitunza na kuilinda kwa ajili ya vizazi hivi na vizazi vijavyo, alisisitiza.

Aliongeza” Ufadhili tunaoutoa sisi ni mdogo sana lakini kazi kubwa na jukumu kubwa ni la jamii yenyewe na Serikali ya Tanzania ndio maana tunapendekeza mbinu hii nzuri itumike na isambae kwenye vijiji na wilaya nyingine nchi nzima”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TFCG, Charles Meshack alisema katika kipindi cha miaka sita katika awamu ya kwanza na ya pili Shirika hilo la ushirikiano na maendeleo ya Uswis limetoa zaidi ya shilingi bilioni 12 na sasa awamu hii ya tatu wametoa kiasi cha shilingi bilioni 7 katika kutekeleza miradi Mradi huu awamu itakayoisha mwaka 2023.

Alisema katika awamu hii ya tatu ambayo imejikita katika kujengea uwezo Wilaya zingine kuanzisha usimamizi shirikishi wa Misitu wameongeza wilaya nne ili nazo ziweze kuambukiza wilaya zingine na hivyo kuwezesha mbinu hiyo kusambaa hatua kwa hatu hadi kufikia nchi nzima.

“Tanzania jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu ambazo hekta milioni  22 sawa na asilimia 45% za misitu hiyo ipo chini ya ardhi za vijiji lakini iliyohifadhiwa chini ya usimamizi shirikishi wa misitu ni asilimia 5 wakati hekta milioni 17 na zisiposimiwa zinaweza kutoweka” alisema Meshack.

Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa Jamii wa usimamizi wa Misitu Tanzania MJUMITA, Rahma Njaidi alisema misitu mingi inaangamia labda ni kwa sababu ya jamii kutojua  thamani na faida za misitu hiyo lakini anaamini baada ya muda mfupi kwa kutumia mbinu hiyo wataona faida na kisha kuwa askari wazuri katika kuilinda na kuitunza Kama ambavyo wanafanya wananchi wa Wilaya ya Kilosa wanaotekeleza mradi huo toka awamu ya kwanza.

“ Kuna vijiji vingi nchi hii ambavyo vina misitu ya miyombo lakini bahati hii imewaangukia nyinyi watu wa Kijiji cha Mahenge wilaya ya Kilolo, hii ni fursa kwenu kuhifadhi na kunufaika na matunda ya uhifadhi shirikishi wa misitu hivyo muwasikilize wataalamu ili muweze kufanikiwa kama wenzenu. “ alisema Njaidi.

Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ) inatekeezwa chini ya Mradi wa kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) na mradi wa kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoFOREAT) kwa ufadhili wa Shirika la  Maendeleo la Uswis (SDC).

No comments:

Post a Comment