Na Vumilia Kondo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi imesema kuna faida nyingi wanazopata kutokana na uwepo wa rasimali ya misitu katika maeneo yao.


Akizungumza mbele ya waandishi wa habari , Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi James Milanzi amesema wilaya yao imebahatika kuwa na misitu mingi ingawa baadhi ya wananchi hawajui faida zake au wanaitumia vibaya.

Milanzi amepongeza Shirika la kuhifadhi misitu ya asili nchini Tanzania (TFCG) pamoja na Mtandao wa jamii wa utunzaji wa misitu (MJUMITA) kwa kuja na mradi wa kuhifadhi misitu kupitia biashara endelevu ya mazao ya misitu ( CoFoREST) kwani ni wakati muafaka wa kutoa elimu hiyo.


Amefafanua kiasili wananchi wao wengi wanajihusisha na kilimo na hasa kilimo cha kuhamahama."Leo wanalima hapa, kesho wanalima kwingine na kila wanapohama wanakwenda kufyeka msitu.Kwa hiyo hii ni changamoto iliyopo ndani ya Wilaya yetu, miradi kama hii ya CoFoREST) inapokuja inasaidia kuelimisha wananchi wetu.

"Mipango hii mizuri ya wadau hao na wengine wengi kwetu  halmashauri inatusaidia, moja kukuza kipato cha wananchi wetu , vijiji ambavyo vimeanza na huu mpango wa matumizi bora ya ardhi sasa wameanza kupata manufaa , kupitia uvunaji wa mazao ya misitu, kwa mwaka wa fedha uliopita tumepata sio chini ya milioni Sh.150.

"Na hiyo ni kutokana na asilimia tano ya kipato chote ambacho kijiji kimepata kutokana na uvunaji misitu, kwa mujibu wa watalaam wanatuambia sasa asilimia inakwenda kuongeza kutoka tano hadi asilimia 10, hivyo mapato yataongezeka.

  "amesema Milanzi.


Kwa upande wake Ofisa Sera na Uraghabishi wa MJUMITA, Elida Fundi amesema "tumekuja na mradi wa kuhifadhi misitu kupitia biashara endelevu ya mazao ya misitu inayofahamika(CoFoREST). Mradi kama huu umekuwa ukitekelezwa katika Mkoa wa Morogoro katika wilaya tatu za Kilosa, Morogoro na Mvomero , tumekuwa tukiutekeleza kwa awamu na sasa tumepata awamu ya tatu itakayokwenda mpaka mwaka 2023.


."Kwa hiyo mradi huu wenyewe sasa tulikuwa tunatekeleza na muundo ambao umelenga katika kuanzisha usimamizi shirikishi katika vijiji pamoja na kuanzisha dhana ya uzalishaji wa mazao ya misitu kwenye usimamizi wa misitu na hii yote inalenga kuhamasisha uhifadhi wa misitu.

"Na kutoa motisha kwa jamii zinazohifadhi misitu waweze kunufaika na ile misitu na kuisimamia kwa nguvu zote na hii imeweza kufanikiwa katika Mkoa wa Morogoro, tukaona tusiishie Morogoro bali twende na wilaya zingine nne.

"Hivyo tumekwenda katika wilaya nyingine nne katika kipindi hiki cha miaka mitatu ikiwemo Wilaya ya Liwale ambako tutakuwa tunatoa mafunzo na kuwa na kijiji cha mfano kimoja.Pia tupo na Wilaya ya Kilolo katika kijiji cha Mahenge,"amesema.


Wakati huo huo Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Liwale Mosses Mkoveke amesema ushiriki wa jinsia katika masuala ya uhifadhi wa misitu umekuwa wa kuridhisha kwani wanaume na wanawake wanashirikiana  vizuri.

"Katika masuala ya misitu kwa sasa wanawake wako sawa na wanaume katika kupata taarifa kuhusu misitu, uongozi na usimamizi wake , katika Kamati za misitu zilizopo vijiji, robo tatu ya wajumbe wote wawe wanawake, na vile vile katika nafasi tatu za uongozi ambazo ni Mwenyekiti , Katibu na Mtunza hazina, mmojawapo asikosekane mwanamke.

"Tumefanya hivyo kwasababu wanawake ni watumiaji wakubwa wa rasilimali zinazotokana na misitu, ndio wanafuata kuni, maji, mbogamboga na matunda yanayopatikana kule porini , kwa hiyo tunatenga muda wa kutosha kuwajenga uwezo kwa wanawake kuweza kutambua na kuthamini na kutenga muda wa kutosha kushiriki, kusimamia na kupanga pamoja maendeleo ya misitu katika vijiji wanavyoishi,"amesema Mkoveke.

Mwisho.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: