FAINALI za mashindano ya urembo nchini maarufu kama 'Miss Tanzania' zinatarajiwa kuhitimishwa Desemba 5, mwaka huu katika ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kampuni ya 'The Look' inayosimamia na kuandaa mashindano hayo Basila Mwanukuzi amesema, hiyo ni mara ya tatu mfululizo kwa Kampuni hiyo kuandaa mashindano hayo, ambayo kwa sasa yanakwenda na kauli mbiu ya "Urembo ni heshima."

"Dkt. Tulia amethibitisha kuwa mgeni rasmi wa shindano hilo na tunaelewa kuwa Naibu spika ni mwanamichezo, mpenda sanaa na kinara katika shughuli zinazoweka kipaumbele katika kusaidia jamii na amekuwa akifuatilia kwa karibu mashindano haya ambayo yanaendeshwa kwa malengo mashindano ya kidunia yaani 'Beauty with Purpose'." Ameeleza.

Amesema, katika mashindano hayo jumla ya walimbwende 20 kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania wamefuzu katika fainali hizo za kumsaka Miss Tanzania.

Basila amesema, licha ya  changamoto ya mlipuko wa ugonjwa wa Korona mwanzoni mwa mwaka, mwitikio ulikuwa mkubwa kwa warembo wengi, wenye vigezo kujitokeza kushiriki mashindano hayo na tayari warembo 20 walioingia katika fainali hizo wana miradi yao ya kusaidia jamii (BWAP) yaani 'Beauty with Purpose Project' ambayo zitashindaniwa na kumpata mshindi.

Share To:

Post A Comment: