Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi akiongea na watendaji wa Idara ya Maendeleo ya  Michezo  ya Wizara hiyo Novemba 24,Jijini Dodoma ambapo amewaagiza kukutana na Wadau wa sekta ya michezo nchini yakiwemo Mashirikisho na Vyama vya Michezo ili kubadilishana utaalamu wa namna ya kuendesha michezo nchini.


Na Shamimu Nyaki-WHUSM, Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi ameiagiza Idara ya Maendeleo ya  Michezo nchini kukutana na Wadau wa sekta hiyo wakiwemo Mashirikisho na Vyama vya Michezo ili kubadilishana utaalamu wa namna ya kuendesha michezo kwa pamoja na kutoa ushauri wa kisera kwa wadau hao.

Dkt. Abbasi ametoa maagizo hayo  Jijini Dodoma katika kikao watumishi wa Idara hiyo ambapo amewataka kusimamia kikamilifu Sekta ya Michezo ambayo inaendelea kuletea heshima Taifa.

“Ni lazima mkutane na Wadau wenu ili mjue wana mawazo gani katika sekta hii na nyie mtoe ushauri wa kitaalamu ambao utaleta tija. Ni lazima muwaeleze wadau Sera ya Michezo inasemaje kwa sababu nyie ndio mnaoisimamia sekta hii “, alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, Katibu Mkuu huyo ameitaka Idara hiyo kuhakikisha kila Shirikisho au Chama cha michezo vinawasilisha Mpango Mkakati wake katika Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambao pamoja na mambo mengine, utaonyesha kalenda ya mwaka katika ligi za kitaifa, kimataifa pamoja na timu ya Taifa . Lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwepo na uelewa wa pamoja kwa wadau wote utakaoleta mafanikio zaidi katika sekta hiyo.

Dkt. Abbasi amesema kuwa Taifa lazima liwe na ushiriki wa mashindano ya michezo ambao utaleta tija, hivyo Idara hiyo ina jukumu la kuhakikisha mashindano yote ambayo nchi inashiriki katika ngazi mbalimbali yanakua na manufaa,  ameongeza kuwa katika mashindano mbalimbali ikiwemo  Olympiki lazima kama nchi kujua aina ya michezo ya kushiriki.

Vilevile, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ni mashindano ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele kwa kuwa yanazalisha vipaji vingi vya michezo mbalimbali nchini. Hivyo, Idara ya Michezo ina jukumu la kusimamia mashindano hayo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo TAMISEMI na Wizara ya Elimu ili vijana wanaofanya vizuri waendelezwe kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya pamoja na sehemu nyingine.

Kwa upande mwingine Katibu Mkuu huyo amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta ya Michezo unaendelea kuimarika ikiwemo kuimarisha Kombe la Mapinduzi.

“Muungano wetu ni muhimu na Kombe la Mapinduzi ni moja ya njia ya kutuunganisha na kuimarisha Muungano wetu, hivyo nitoe rai kwa Vilabu kupeleka timu bora katika mashindano hayo”alisema Dkt.Abbasi.

Akiongelea kuhusu miuondombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja, Dkt. Abbasi ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza na matarajio ni kuwa na viwanja bora vya  michezo nchini na tayari Ujenzi wa Uwanja wa  Dodoma umefikia hatua nzuri.

Share To:

Post A Comment: