Monday, 23 November 2020

Benki ya CRDB yazindua Mashine ya Kubadili Fedha za Kigeni (FOREX ATM)

 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mashine ya kubadili fedha ya Benki ya CRDB. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha Benki Kuu, Jerry Sabi (wapili kulia) na Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati Benki ya CRDB, Boma Raballa (wakwanza kushoto), Meneja wa Kanda ya Kaskazini Benki ya CRDB, Chiku Issa (wakwanza kuli). Uzinduzi huo ulifanyika katika tawi la Benki ya CRDB Meru jijini Arusha wikiendi iliyopita.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta akisoma risiti muamala baada ya kubadili dola za kimarekani katika mashine ya kubadili fedha ya Benki ya CRDB. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha Benki Kuu, Jerry Sabi (watatu kushoto) na Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wa pili kulia). Uzinduzi huo ulifanyika katika tawi la Benki ya CRDB Meru jijini Arusha wikiendi iliyopita.

=====  =====  =====

Arusha – 21 Novemba, 2020 - Benki ya CRDB imezindua mashine ya kubadili fedha za kigeni “FOREX ATM” katika tawi lake la Meru lililopo jijini Arusha. Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha huduma hiyo huku akisema uwepo wa huduma hiyo utasaidia kuchochea shughuli za utalii na biashara kwa ujumla katika mkoa.

“Niwapongeze kwa ubunifu huu mliokuja nao ambao utasaidia kuwezesha wateja kupata huduma ya kubadili fedha masaa 24 kupitia mashine hii,” alisema Kimanta huku akionyesha kufurahishwa na urahisi wa kutumia mashine hiyo ya kubadili fedha.

Kimanta aliwataka wakazi wa Arusha kuchangamkia fursa hiyo ya kubadilisha fedha kupitia mashine hiyo ya kubadili fedha ya Benki ya CRDB, huku akiwataka kuachana na utaratibu wa kubadili fedha sehemu zisizo rasmi.

Akitoa hotuba yake Afisa Mkuu wa Uendeshaji Benki ya CRDB, Bruce Mwile alisema lengo la kuanzishwa kwa huduma ya mashine ya kisasa ya kubadili fedha za kigeni ni kuwawezesha wateja na wale wasio wa benki hiyo kubadilisha fedha za kigeni kwa urahisi na haraka. 

“Lengo letu nikuhakikisha mteja anapata huduma bora na kwa wakati, na hii inafikiwa kwa kuwekeza katika teknolojia sahihi ambayo inarahisa upatikanaji wa huduma kama ilivyo kwamashine hii ya kubadili fedha za kkgeni,” anasema Bruce.

Bruce anasema kutumia huduma hiyo ya mashine ya kubadili fedha mteja anatakiwa kutembelea mashine hiyo akiwa na hati ya kusafiria (Pasipoti), atachagua huduma ya kubadilisha fedha na kisha kufuata maelekezo yatakayomuwezesha kubadili fedha.

“Kwa kuanzia mteja anaweza kubadili fedha 3 za kigeni ikiwamo Dola ya Marekani (USD), Paundi ya Uingereza (GBP) na fedha ya Ulaya (Euro), lakini tunategemea kuongeza fedha zaidi siku za hivi karibuni,” ansema Bruce huku akibainisha kuwa Benki hiyo pia ipo katika mchakato wa kuwezesha kitambulisho cha taifa (NIDA) kutumika kama mbadala wa hati ya kusafiria kupata huduma hiyo.

“… tunatambua Watanzania wengi bado hawana hati ya kusafira, kitambulisho cha NIDA kitasaidia sana kwa Watanzania wengi kupata huduma,” anasema Bruce.

Naye Mkurugenzi wa Usimamizi Sekta ya Fedha Benki Kuu, Jerry Sabi aliipongeza Benki ya CRDB kwa uzinduzi wa huduma hiyo ya mashine ya kubadili fedha huku akibainisha kuwa mashine hiyo itasaidia kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya kubadili fedha katika mazingira salama na kwa uhakika zaidi.

Sabi ameitaka Benki ya CRDB kuendelea kusambaza mashine hizo za kubadili fedha nchi nzima hasa katika maeneo ya kimkakati kama katika viwanja vya ndege, bandarini, mipakani na maeneo ya kibiashara, ili kuendana na mahitaji yaliyopo katika soko.

“Najua hili la kusambaza mashine hizi nchi nzima lipo ndani ya uwezo wenu, basi niwaombe mfanye hivyo ili sehemu zote za Tanzania waweze kunufaika. Nitoe rai kwa benki nyengine kuwekeza kwenye teknolojia ya namna hii na sisi Benki Kuu tutaendelea kuweka mazingira wezeshi,” anasema Sabi.

Sabi pia aliipongeza Benki ya CRDB kwa namna ambayo imekuwa ikiwekeza katika miundombinu ya utoaji huduma kwa wateja hususani CRDB Wakala ambao wamesambaa nchi nzima na hivyo kurahisha upatikanaji wa huduma za benki hiyo kwa wateja. 

“… tumemsikia hapa Afisa Mkuu wa Uendeshaji akisema sasa hivi mna zaidi ya CRDB Wakala 17,000. Niwaombe kasi hii pia muende nayo katika mashine hizi za kubadili fedha za kigeni,” aliongezea Sabi.

No comments:

Post a Comment