Mkuu wa Mkoa wa Singida (RC) Dkt Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwalimu Mstaafu kutoka Wilaya ya Singida  Amosi Njoghomi kiasi cha shilingi milioni 18.8 zilizookolewa kutoka kwa mmoja wa wakopeshaji wa ‘Riba Umiza.’ Mwalimu Njoghomi alikopa shilingi milioni 2, lakini mkopeshaji alimtaka arejeshe fedha taslimu shilingi milioni 31 hadi serikali ilipoingilia kati na kumsaidia. 

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Singida, Suzan Shesha (kulia) akishuhudia tukio la Mwalimu Njoghomi kukabidhiwa pesa zilizookolewa. Kushoto ni Mwenyekiti Mstaafu wa CWT mkoa wa Singida, Aran Jumbe.
Familia ya Mwalimu Mstaafu Albert Mpahi ikipokea kiasi cha shilingi milioni 2 zilizookolewa kutoka kwa moja ya Kampuni za Mikopo zisizofuata utaratibu. Mwalimu Mpahi alikopa shilingi milioni 7.2 na mkopeshaji wake akamtaka arejeshe fedha taslimu Shilingi Milioni 17 hadi serikali ilipoingilia kati.
RC Nchimbi akimkabidhi Mwalimu Mstaafu kutoka Wilaya ya Ikungi  Gerase Mshumbusi kiasi cha shilingi milioni 13 zilizookolewa kutoka kwa mmoja wa wakopeshaji wa ‘Riba Umiza.’ Mwalimu Mshumbusi alikopa shilingi milioni 3.5, lakini mkopeshaji alimtaka arejeshe fedha taslimu shilingi milioni 17 hadi serikali ilipoingilia kati na kumsaidia.
Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Singida Suzan Shesha (kushoto) akishuhudia tukio la Mwalimu Gerase Mshumbusi kukabidhiwa pesa zilizookolewa. Kulia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CWT mkoa wa Singida, Aran Jumbe.
RC Nchimbi akizungumza na wadau mbalimbali kutoka kwenye mabenki, Taasisi, Maafisa Utumishi, watu binafsi na Kampuni za Mikopo kutoka mkoa wa Singida kabla ya zoezi la kurudisha fedha zilizookolewa.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, akitoa taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba 2020.
Wadau wakifuatilia mkutano huo .
Mkutano ukiendelea.
Maombi na Dua maalumu kupitia mkutano huo vikifanyika kwa lengo la kuliombea Taifa la Tanzania na watu wake.
Maombi yakiendelea.
Familia ya Mwalimu mstaafu Albert Mpahi muda mfupi baada ya kukabidhiwa shilingi milioni 2 zilizookolewa na serikali.


 Na Godwin Myovela, Singida


RAIS John Magufuli amewafuta machozi walimu, wastaafu na baadhi ya wananchi mkoani hapa kwa kuokoa na hatimaye kuwakabidhi mali na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 82 walizokuwa wametapeliwa kupitia Kampuni za Mikopo zinazoendesha shughuli zake kinyume na utaratibu.

Mkuu wa Mkoa Dk Rehema Nchimbi, kwa niaba ya Rais, amewakabidhi kiasi hicho cha fedha waathirika wote waliopitiwa na wimbi hilo, maarufu ‘Mikopo Umiza,’ ofisini kwake leo.

“Ni Serikali hii ya Magufuli ndio iliyofanikisha kuwabana hawa wakopeshaji haramu na hatimaye leo walimu wangu na ninyi watumishi wenzangu mnakabidhiwa haki yenu iliyokuwa imeporwa, tuendelee kumshukuru Rais kwa mema haya anayoendelea kutufanyia,” alisema Nchimbi na kuongeza:

“Rais Magufuli mda mrefu alishakampeniwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe kupitia Corona, kama Mungu alipitishia kwake ile neema, maono na uwezo ule wa kusimama bila kutetereka, mimi Rehema Nchimbi ni nani hata nisiendelee kumsifu?” alihoji.

Akiwasilisha taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema takribani shilingi milioni 82.8 pamoja na mali nyingine vimeokolewa na kurejeshwa kwa wahusika. 

Alisema matokeo ya ufuatiliaji na udhibiti huo umebaini kuwa baadhi ya wakopeshaji binafsi wanafanya shughuli hiyo bila ya vibali halali, hali inayosababisha kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato na kujipatia fedha isivyo halali.

Pamoja na mambo mengine, alisema udhibiti umebaini kuwepo kwa utozaji mkubwa wa riba zisizovumilika za zaidi ya asilimia 100 kinyume na viwango vilivyowekwa na kuainishwa na Benki Kuu, sanjari na wakopeshaji kukaa na kadi za benki za wakopeshwaji kwa lengo la kuchukua fedha kila ifikapo mwisho wa mwezi. 

Aidha, kupitia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Takukuru, imeelezwa baadhi ya wakopeshaji hawaandai mikataba ya ukopeshaji, hivyo wakopeshwaji hawana nakala za mikataba, na hata iliyopo kwa baadhi ya kampuni hizo haikidhi sifa na vigezo.

“Baadhi ya kampuni hizi za mikopo hazina hata wataalamu wa mahesabu hali inayowafanya kutoza riba zenye mkanganyiko, na hivyo kujikuta wakimbambikiza riba kubwa mkopeshwaji,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Hata hivyo, Afisa wa Takukuru mkoani hapa, Shemu Mgaya, pamoja na mambo mengine alisema kuna uvujaji mkubwa wa taarifa za watumishi wanaostaafu. Mathalani mafao ya mstaafu yanapokuwa yameingizwa benki wakopeshaji wanakuwa wa kwanza kupata taarifa kabla ya mhusika. 

“Tumebaini kwa baadhi ya mabenki kuna ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kibenki kupitia maafisa wao, kwa eneo la kuwezesha kutolewa fedha kutoka akaunti ya mteja kwenda akaunti ya mkopeshaji bila mwenye akaunti kuwepo,” alisema Mgaya na kuongeza: 

“Udhibiti pia umebaini hata Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikichelewesha mafao kwa wastaafu hali ambayo inasababisha baadhi ya wastaafu kujikuta wakiingia katika hii mikopo umiza (mikopo yenye riba kubwa).” 

Ofisi hiyo ya Takukuru, hata hivyo inasisistiza kuwa endapo matokeo hayo ya udhibiti na mapendekezo yatatekelezwa basi ni dhahiri yataleta ustawi kwa wazee na wastaafu wa Tanzania ikizingatiwa wastaafu ndio ‘Hazina ya Taifa.’


FUATILIA HAPA CHINI TAARIFA ALIYOPOKEA MKUU WA MKOA KWA NIABA YA RAIS YA KAZI KUBWA YA ILIYOFANYWA NA TAKUKURU KUWABANA WAKOPESHAJI HARAMU NA KULINDA MASLAHI YA WANYONGE KWENYE WILAYA ZA SINGIDA, IRAMBA, IKUNGI NA MANYONI KUFUATIA AGIZO LA HIVI KARIBUNI 

 

26 Oktoba, 2020

 

TAARIFA YA FEDHA ZILIZOOKOLEWA NA TAKUKURU MKOA WA SINGIDA KUTOKANA NA RIBA UMIZA KIPINDI CHA JULAI HADI OKTOBA,2020

MKOA WA SINGIDA.

  1. WILAYA YA SINGIDA

a.       Wilaya ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 18,800,000/= kutoka kwa Mkopeshaji BISEKO MUNGETA KAZUNGU ambaye alimkopesha Mwalimu Mstaafu AMOSI NJOGHOMI fedha kiasi cha Tshs.2,000,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha Tshs. 31,000,000/=.Tunaomba leo Fedha hizi Tshs. 18,800,000/= uzikabidhi kwa  AMOSI NJOGHOMI.

b.      Wilaya ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 700,000/= kutoka kwa Mkopeshaji CHARLES WAWA ambaye alimkopesha Mtumishi Mmoja wa serikali (Jina limehifadhiwa) fedha kiasi cha Tshs.500,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha Tshs.1,900,000/=.Fedha hizi zimekabidhiwa kwa mhusika kupitia Akaunti yake huku tukiendelea kufuatilia fedha iliyosalia.

c.       Wilaya ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 2,000,000/= kutoka kwa Kampuni ya BOMANG MICROFINANCE ambayo ilimkopesha Mwalimu Mstaafu ALBERT SUNGI MPAHI fedha kiasi cha Tshs.7,200,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha Tshs.17,000,000/=. Tunaomba leo Fedha hizi Tshs. 2,000,000/= uzikabidhi kwa  ALBERT SUNGI MPAHI, TAKUKURU inaendelea kufuatilia fedha zilizosalia.

IKUNGI

a.       Katika  Wilaya ya IKUNGI tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs.17,000,000/= kutoka kwa mkopeshaji , kampuni ya MAGIREI COMPANY LTD (MICRO CREDIT) ya Singida mjini. Kampuni hii ilimkopesha Mwalimu Mstaafu GERASE KAJUNA MSHUMBUSI Tsh.3,500,000/= mwaka 2015 na kulipa Tsh.17,000,000/=  mwaka 2017. Baada ya Ofisi ya TAKUKURU kufanya ufuatiliaji iliitaka kampuni hii imrejeshee jumla ya Tshs.17,000,000/=. BWANA GERASE KAJUNA MSHUMBUSI alirejeshewa kupitia kwenye akaunti yake namba 50802500415 iliyopo katika Benki ya NMB kiasi cha Tsh.4,000,000/=  kati ya tarehe 02/07/2020 na tarehe 03/08/2020. Tunaomba leo Fedha iliyosalia kiasi cha Tshs. 13,000,000/= uzikabidhi kwa Mwalimu Mstaafu GERASE KAJUNA MSHUMBUSI .

b.      Kampuni iitwayo WIDOP COMPANY LTD ilimkopesha kiasi cha Tsh.1,700,000/= Bi. LUCIA PETRO NYIKA Muuguzi Mstaafu na kurejesha kiasi cha Tsh.5,100,000/=  .Baada ya TAKUKURU kufuatilia Bi. LUCIA PETRO NYIKA amerejeshewa Tshs.2,400,000/=  tarehe 15/10/2020, na fedha nyingine zilizobaki zipo kwenye utaratibu wa kurejeshwa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi na mara tu zitakaporejeshwa atakabidhiwa Bi. LUCIA PETRO NYIKA.

IRAMBA       

a.       TAKUKURU (W) ya  IRAMBA imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.3,500,000/= zilizokuwa zimechukuliwa na kampuni ya ANGELVA FINANCIAL LTD kinyume na utaratibu wa Kibenki. Ambapo  siku ya  tarehe 26/06/2020 Ofisi ya TAKUKURU (W) IRAMBA ilimkabidhi MAGRETH  BUSONGO fedha  kiasi cha Tsh.3,500,000/=.

Awali ilipokelewa taarifa ya  kulipishwa riba kubwa katika mkopo aliokopa kutoka kwa kampuni ya ANGELVA FINANCIAL LTD ya Kiomboi Iramba kiasi cha Tsh.1,000,000/= mwezi agosti mwaka 2019  na kulipa marejesho ya Tsh.9,250,000/= mwezi February mwaka 2020 sawa na riba ya asilimia 925 baada ya kupata fedha za mafao ya kustaafu.

 

MANYONI

a. TAKUKURU(W) YA  MANYONI imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.360,000/= zilizokuwa zimechukuliwa na kampuni ya MWITA CREDITORS kinyume na utaratibu wa Kibenki .Mtumishi Mstaafu Bw. CHRISTOPHER MWALUKO KABUDI alizidishiwa riba kwenye mkopo wake na alikuwa amelipa fedha nyingi kuliko alivyotakiwa kurejesha.Baada Takukuru kufuatilia ilibainika kwamba kiasi cha shilingi laki tatu na sitini (360,000/=) zilikua zimerejeshwa na mlalamikaji baada ya mkopo kumalizika.Hivyo wahusika walipohojiwa walikiri kosa na kuzirejesha fedha hizo kiasi cha Tshs. 360,000/=. TAKUKURU(W) ya Manyoni imerejesha fedha hizo kwa CHRISTOPHER MWALUKO KABUDI.

b.      TAKUKURU (W) MANYONI imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.200,000/= zilizokuwa zimechukuliwa na ALPHONCE NJALIKE kinyume na utaratibu wa Kibenki. Bi.PAULINA JOSEPH alikopa kwa ALPHONCE NJALIKE kiasi cha shilingi laki mbili na wakati wa marejesho alishindwa kurejesha waliuza vitu vyake vya ndani yakiwemo makochi.Baada ya ofisi kuingilia kati iligundua kwamba mkopeshaji hakuwa na leseni ya ukopeshaji na pia taratibu za uuzwaji wa makochi yake haukufuatwa.Baada ya mlalamikiwa kuhojiwa na ofisi aliomba kulipa gharama za makochi hayo kiasi cha shilingi laki mbili (200,000/=) na hivyo kufutwa kwa deni husika na mlalamikaji kupata haki yake.

 

c.       TAKUKURU (W) MANYONI ilifanya ufuatiliaji kwa ISSA KIULA BAKARI ni Mwalimu mstaafu na alitozwa riba kubwa na  HAMIS ISSA ambae awali alikuwa mfanyakazi wa MRITHOS CREDITORS. Alikopa kiasi cha shilingi milioni tisa (Tshs. 9,000,000) pamoja na riba na wakati wa marejesho mlalamikiwa alikua na kadi pamoja na namba ya siri ya mlalamikaji.

Kutokana na hivyo mlalamikiwa alichukua kiasi cha shilingi milioni kumi na nane kwenye akaunti ya mlalamikaji. Baada ya mlalamikaji kumfuata alikubali kulipa shilingi milioni tatu.Takukuru ilifanya ufuatiliaji na mlalamikiwa nae alikiri kuwa na kiasi cha shilingi milioni tano na laki tano (Tshs.5,500,000/=) za mlalamikaji. Aliomba kuzilipa fedha hizo ndani ya mwezi mmoja na tayari ameshalipa shilingi milioni nne (Tshs.4,000,000/=) ambazo mlalamikaji ISSA KIULA BAKARI alikabidhiwa na Katibu Tawala wa Wilaya Manyoni. .Fedha zilizobaki zitawasilishwa TAKUKURU na mdaiwa tarehe 29 mwezi huu wa Oktoba 2020.

TAKUKURU (M) inazidi Kutoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya Rushwa na kushiriki kikamilifu kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwa kufika ofisi zetu za TAKUKURU (M) na Wilaya au kupiga simu namba 113, kwa kutumia TAKUKURU APP wanapobaini kutokea/kutaka kutokea kwa vitendo vya Rushwa na kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani.

Imetolewa na:

 

ADILI ELINIPENDA

MKUU WA TAKUKURU (M)

SINGIDA


Share To:

Post A Comment: